Mahakama ya ICC yatoa hati za kukamatwa kwa aliyekuwa  waziri wa ulinzi wa zamani wa Urusi Sergei Shoigu na jenerali mkuu wa Urusi Valery Garasimov. /Picha: Reuters

Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ilitoa hati za kukamatwa kwa Sergei Shoigu, waziri wa zamani wa ulinzi wa Urusi, na jenerali mkuu wa Urusi Valery Gerasimov. Jumanne kwa tuhuma za uhalifu uliofanywa wakati wa uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

Hadi sasa hati nane za kukamatwa zilitolewa dhidi ya washukiwa wakuu wa Urusi tangu Moscow ilipotuma wanajeshi nchini Ukraine mnamo Februari 2022. Rais wa Urusi Vladimir Putin, ni kati ya wale ambao wanakabiliwa na mashtaka ya kusafirisha watoto wa Ukraine hadi Urusi.

Hatua ya mahakama ilikaribishwa na Kyiv, lakini ikatupiliwa mbali na Moscow kuwa haina maana kisheria. Mahakama hiyo yenye makao yake mjini Hague ilisema Shoigu na Gerasimov walishukiwa kufanya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu kwa kuelekeza mashambulizi dhidi ya raia na vitu vya kiraia nchini Ukraine.

Majaji waligundua kuwa kulikuwa na "sababu nzuri za kuamini kwamba washukiwa hao wawili waliwajibika kwa mashambulizi ya makombora yaliyofanywa na jeshi la Urusi dhidi ya miundombinu ya umeme ya Ukraine" kati ya Oktoba 10, 2022 na angalau Machi 9, 2023, ICC ilisema kupitia taarifa kwa vyombo vya habari.

Urusi, ambayo si mwanachama wa ICC, imesema mara kwa mara miundombinu ya nishati ya Ukraine ni shabaha halali ya kijeshi na inakanusha kuwa inalenga raia au miundombinu ya kiraia.

Ukraine pia si mwanachama, lakini imeipa ICC mamlaka ya kushtaki uhalifu uliofanywa katika eneo lake tangu Novemba 2013. Kyiv ilipongeza hatua ya kutoa hati za kukamatwa.

"Kila mhalifu anayehusika katika kupanga na kutekeleza mashambulizi dhidi ya Ukraine lazima ajue kwamba haki itatendeka," Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy alisema. "Na tunatumai kuwaona wamekamatwa."

Baraza la Usalama la Russia limesema hatua hiyo ya mahakama ni sehemu ya vita vya propaganda dhidi ya Moscow. "Hii ni kama kufyetua risasi kwenye hewa tu, kwa vile mamlaka ya ICC hayana mamlaka ya kushtaki Urusi, na yalifanywa kama sehemu ya vita vya propaganda vya nchi za Magharibi dhidi ya nchi yetu," shirika la habari la serikali TASS lilinukuu baraza hilo likisema.

Kwa kuwa ICC haina jeshi la polisi la peke yake na inategemea nchi wanachama kukamata washtakiwa, haijulikani ikiwa washukiwa wa Urusi watawahi kushtakiwa.

Kwa mujibu wa majaji wa ICC, kulikuwa na sababu za kuridhisha za kuamini kwamba mashambulizi hayo yalilenga zaidi raia na miundombinu ya raia.

Reuters