Wapiganaji wa Wagner wakiondoka Rostov-on-Don / Picha: Reuters

Yevgeny Prigozhin, mkuu wa kundi la mamluki la Wagner la Urusi, alionekana akiondoka katika makao makuu ya kijeshi katika mji wa Rostov-on-Don kwa gari aina ya SUV.

Alionekana katika video iliyowekwa kwenye Telegram na shirika la habari la serikali ya Urusi, RIA.

Prigozhin hapo awali alikubali kukomesha uasi dhidi ya uongozi wa kijeshi wa Moscow baada ya upatanishi kutoka kwa rais wa Belarus Alexander Lukashenko, na Kremlin ilisema kuwa atahamia Belarus chini ya makubaliano waliyofanya.

Prigozhin ambaye aligeuza kikosi chake cha Wagner dhidi ya uongozi wa kijeshi huko Moscow, ataondoka kuelekea Belarus na kesi ya jinai dhidi yake itafutwa, Urusi ilisema mapema Jumapili.

"Kuepuka umwagaji damu, mizozo ya ndani, na migongano na matokeo yasiyotabirika lilikuwa lengo kuu ya maamuzi haya ," msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov aliwaambia waandishi wa habari.

Chini ya makubaliano hayo, yaliyosimamiwa na Lukashenko, wapiganaji wa Wagner hawatashtakiwa, Peskov aliongeza.

"Siku zote tumeheshimu matendo yao ya kishujaa mbele." "Makubaliano yamefikiwa kwamba wapiganaji wa Wagner watarejea katika kambi zao," Peskov alisema, akiongeza kuwa wapiganaji ambao hawakushiriki katika uasi huo wataruhusiwa kujiunga rasmi na jeshi la Urusi.

Haijulikani ikiwa Prigozhin alipata makubaliano spesheli.

Peskov alikataa kusema ikiwa kulikuwa na makubaliano yoyote spesheli na Prigozhin, zaidi ya uhakikisho wa usalama wake.

"Hakuna masharti zaidi ambayo ninaweza kukuambia," Peskov alisema.

TRT Afrika