Bob Marley bado ana umaarufu mkubwa miaka 42 baada ya kifo chake / Photo: Getty Images

Na Brian Okoth

Ushawishi wa Bob Marley unaendelea kuongezeka miaka 42 baada ya kifo chake.

Kwenye mtandawo wa kijamii wa Facebook, kuna kurasa zilizoanzishwa miaka mingi baada ya kifo chake, msanii huyo mashuhuri wa Jamaica ana wafuasi milioni 67.1.

Kurasa hizo za mitandawo za kijamii zinasimamiwa na timu inayoitwa ‘jumuiya ya mashabiki wa Bob Marley’ ambayo huchapisha mara kwa mara mambo kumhusu - labda ili kuweka hai historia tajiri ya mwanamuziki huyo.

Mwanahabari Nzau Musau, Mhariri wa shirika kongwe zaidi la habari nchini Kenya linaloitwa The Standard, anasema urithi wa Marley umekuwa wa kudumu kwa sababu maisha yake na muziki hutia matumaini.

Katika Twitter, mwanamuziki huyu marehemu pia anawafuasi milioni 1.4, na milioni 7.2 kwenye mtandawo wa Instagram.

"Maisha ya Bob, hadithi na muziki, ni hadithi ya matumaini, uthabiti na ushindi. Angalia historia yake... maskini, aliyekata tamaa, aliyekataliwa lakini kupitia bidii, umakini, na imani katika kujitolea, anashinda yote hayo na kuwa mwimbaji nyota wa kwanza wa reggae duniani,” Musau, shabiki mkubwa wa Mjamaica huyo, aliiambia TRT Afrika.

"Pia ni hadithi ya kusikitisha ya hali mbaya ya mafanikio ya muziki, na kila kitu ambacho kinaweza kuharibika kwa umaarufu, na ufuasi wa kishupavu. Kwa maneno ya mshauri wake, Lee Scratch Perry, 'Nampenda sana Bob, ni aibu',” aliongeza.

Siri ya uimara wa Marley baada ya kufa, kulingana na Musau, ni uwezo wake wa "kuchanganya akili na ushabiki kwenye nyimbo", na hiyo "inaifanya kuwa nzuri".

"Mara tu unapoanza kutilia maanani maneno ya Bob katika nyimbo zake, unavutiwa," alisema. Licha ya kuungwa mkono sana barani Afrika, safari ya kwanza ya Marley katika bara hilo ilikuja mnamo Desemba 1978.

Ziara ya Kwanza ya Bob Marley barani Afrika ilikuwa nchini Ethiopia 

Kama ilivyotarajiwa ziara yake ya kwanza Afrika ilikuwa jiji la Addis Ababa nchini Ethiopia - nyumbani kwa Haile Selassie, ambaye anachukuliwa na marastafari kama mungu wa jamii ya watu weusi.

Rastafari wanaamini kwamba mwangalizi mkuu wa ulimwengu, Mungu, ni mweusi. Wakati wa ziara yake nchini ethiopia , Marley alikaa Shashamane, makaazi ya jumuiya ambayo yalikuwa yametolewa kwa rastafari na mfalme wa Ethiopia wa zamani, Haile Selassie.

Katika wasifu wa Marley, ulioandikwa na Stephen Davis, mwimbaji huyo nyota wa reggae aliwahi kusema: "Ninajua kwamba ukuu wake wa kifalme, Mfalme Haile Selassie wa Ethiopia ndiye mwenyezi... Sioni ni kiasi gani watu wetu wanataka kushawishiwa zaidi."

Mjane wa mwanamuziki huyo, Rita, alinukuliwa na gazeti ya ‘The Guardian’ akisema kwamba maisha ya Marley yalikuwa "kuhusu Afrika, na si Jamaica".Kulingana na Rita, "Ethiopia ni mahali pa kupumzika kiroho kwa Marley".

Alikuwa amepelekwa katika hospitali ya Jackson Memorial huko Miami, Florida, Marekani, alipofariki akipatiwa matibabu.

Ili kudumisha uhusiano wa baba yao na Ethiopia, watoto wa Marley, akiwemo Damian, mara nyingi wametembelea taifa hilo la Kiafrika, wakitumbuiza mashabiki huko mara kadhaa.

Katika safari yake ya kwanza barani Afrika mnamo Desemba 1978, Bob Marley alisimama kwa muda nchini Kenya alipokuwa akielekea nchi jirani ya Ethiopia.

Uhusiano na Zimbabwe

Mbali na Ethiopia, Bob Marley alitembelea Zimbabwe na Gabon.

Aliheshimiwa sana nchi ya Zimbabwe hivi kwamba nchi hiyo ilipopata uhuru mnamo Aprili 18, 1980, alikuwa mtumbuizaji pekee wa kigeni aliyealikwa kutumbuiza wakati wa sherehe za Siku ya Uhuru jijini Harare.

Marley, ambaye alivutiwa na ukombozi wa Zimbabwe, hata alitunga wimbo kwa heshima ya nchi hiyo.

Ili kuonyesha jinsi alivyokuwa na hamu ya uhuru wa Zimbabwe, alijilipia tikiti yake ya ndege, na kwenda katika taifa hilo la Afrika licha ya hatua hiyo kupingwa na usimamizi wake.

Raia wa Zimbabwe walifurahishwa sana na uwepo wa Marley kiasi kwamba polisi walilazimika kurusha vitoa machozi ili kuzuia majaribio ya kuingia kwenye Uwanja wa Rufaro.

Ili kuwatuliza wale ambao walikuwa wamenyimwa kuingia katika tamasha, siku iliyofuata - Aprili 19, 1980 - Marley alitumbuiza kwa hadhira ya zaidi ya watu 100,000.

Bob Marley pia alitembelea Zimbabwe na Gabon

Mtoto wa rais

Mahusiano yake na Gabon yalikuwa ya kuvutia. Imeripotiwa sana kuwa Marley alipendana na bintiye rais wa pili wa Gabon, Omar Bongo.

Pascaline Bongo alikuwa mwanafunzi wa chuo kikuu nchini Marekani mwenye umri wa miaka 23 mwishoni mwa miaka ya 1970, alipokutana na Marley, ambaye alikuwa nchini humo kwa tamasha.

Pascaline alikuwa amehudhuria onyesho la mwanamuziki huyo huko Los Angeles, na msichana huyo alivutia macho ya msanii huyo. Wawili hao wakaendelea kuwasiliana, na Pascaline akamualika Marley kutumbuiza katika nchi yake ya asili ya Gabon.

Mwanamuziki huyo, baadaye, aliimba kwenye uwanja wa Gymnase Omnisport Bongo huko Libreville mnamo Januari 4 na 6, 1980.

Katika kitabu kiitwacho ‘Bob Marley and the Dictator’s Daughter’, mwandishi wa habari Mfaransa Anne-Sophie Jahn anamnukuu Pascaline akisema kwamba yeye na Marley walifurahia “mapenzi lakini hayakuwezekana” kwa sababu ya haiba na asili zao tofauti.

Wawili hao, hata hivyo, waliendelea na mapenzi yao hadi kifo cha Marley. Msanii huyo wa Jamaica, ambaye jina lake la kuzaliwa ni Robert Nesta Marley, angesherehekea siku yake ya kuzaliwa ya 78 mnamo Februari 6, 2023.

Akiwa na mafanikio makubwa katika muziki, Marley alipokea Medali ya tatu ya amani ya Umoja wa Mataifa, alitunukiwa katika jumba la umaarufu la Rock and Roll mwaka 1994; na mwaka wa 2001, alitunukiwa Tuzo ya mafanikio ya maisha katika tuzo ya kimataifa ya Grammys.

Nyimbo zake maarufu ni pamoja na ‘No Woman No Cry’, ‘Redemption Song’, ‘Satisfy My Soul’, ‘Sir It Up’ na ‘One Love’. Hadi sasa Marley, bila shaka, anasalia kama mwanamuziki mkuu wa reggae kuwahi kuishi.