| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
Jaji Chande: Vifo baada ya vurugu za uchaguzi vimeacha pengo kubwa
Kulingana na Jaji Mstaafu Chande, mkoa wa Dar es Salaam unaongoza ukiwa na idadi ya vifo 182, ikifuatiwa na Mwanza ambayo ilikuwa na vifo 90, Mbeya vifo 80 na mkoa wa Arusha ukiwa na vifo 53.
Jaji Chande: Vifo baada ya vurugu za uchaguzi vimeacha pengo kubwa
Matokeo ya Tume hii yamekuwa yakisubiriwa kwa hamu tangu kuundwa kwake na Rais wa Tanzania Novemba 18, 2025./Picha:@ikulumawasliano

Ripoti ya Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani wakati na baada ya uchaguzi  mkuu wa Oktoba 29, 2025 nchini Tanzania, imekiri kwamba vifo vilivyotokea wakati huo vimeacha pengo kubwa kwa familia hivyo kusababisha athari za kiuchumi na utegemezi katika jamii.

Ripoti hiyo iliwasilishwa Aprili 23, 2026 na Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman kwa kiongozi wa nchi hiyo, Samia Suluhu Hassan, ikulu jijini Dar es Salaam.

"Idadi ya vifo 518 inaweza kuwa sio ya mwisho kwani baadhi ya watu au ndugu zao waliamua kwenda kutibiwa maeneo binafsi," amesema Jaji huyo Mkuu Mstaafu.

Kulingana na Jaji Mstaafu Chande, mkoa wa Dar es Salaam unaongoza ukiwa na idadi ya vifo 182, ikifuatiwa na Mwanza ambayo ilikuwa na vifo 90, Mbeya vifo 80 na mkoa wa Arusha ukiwa na vifo 53.

Hii ni mara ya kwanza kwa serikali kupitia chanzo rasmi kutoa idadi ya watu waliopoteza maisha wakati wa vurugu hizo.  Hata hivyo, takwimu hizi, zimetiliwa mashaka, kufuatia madai ya kuwepo kwa idadi kubwa ya watu wanaodaiwa kufariki.

Matokeo ya Tume hii yamekuwa yakisubiriwa kwa hamu tangu kuundwa kwake na Rais wa Tanzania Novemba 18, 2025.

Tume hiyo ilikuwa ilipewa muda wa siku 90 kukamilisha ripoti yake, hata hivyo, baadae iliongezewa muda wa uwasilishaji hadi Aprili 27, badala ya ile ya awali ya Aprili 3, 2026.

Wakati wa uchunguzi wake, tume hiyo ilitumia siku 153, ikifanya mahojiano na watu 63, 603.

CHANZO:TRT Afrika Swahili