Begi lililoachwa na mshukiwa katika kituo cha treni cha Berlin lilisheheni vilipuzi, kwa mujibu wa polisi / Picha : Reuters

Polisi Ujerumani wamefanya msako zaidi Alhamisi asubuhi wakimtafuta mtu mmoja aliyekimbia kufanyiwa ukaguzi wa kawaida katika kituo cha treni mjini Berlin, na kuacha furushi la vilipuzi.

Tukio hilo limetokea Jumatano jioni katika kituo cha treni cha Neukolln baada ya mtu mmoja kukimbia pindi polisi walipomsimamisha na kutaka kukagua kitambulish chake, imesema polisi Berlin katika taarifa yake.

Begi lililoachwa na mshukiwa lilisheheni vilipuzi, kwa mujibu wa polisi. Vyombo vya habari vimeripoti kuwa vilipuzi hivyo vilikuwa ni triacetone triperoxide (TATP). Wataalamu wa kuzibua mabomu walivisafirisha vilipuzi hivyo kwa tahadhari katika bustani iliyopo karibu na kufanikiwa kuvizibua.

Wachunguzi pia wamepata kitambulisho cha mtu mwenye miaka 30 raia wa nchi ya Poland. Hata hivyo, polisi imesema kitambulisho hicho kipo katika orodha ya vitambulish vilivyopotea tangu Januari 2022.

Uchunguzi wa awali hauonyeshi kufanana kwa mshukiwa huyo na picha iliyopo katika kitambulisho, shirika la umma la RBB limeripoti.

AA