Tangu Juni 25, Vijana wa Kenya maarufu kama Gen Z wamekuwa wakifanya maandamano kupinga kuongezwa ushuru na hali ngumu ya maisha / Picha : Reuters 

Na Dayo Yussuf

Kuna methali ya Kiswahili isemayo ‘Ukiona mwenzako anyolewa, chako tia maji’.

Onyo hilo ingawa katika lugha tofauti linaweza kuvuka mipaka kwa urahisi haswa kwa kuwa yote yanayotokea siku hizi yanaonekana mubashara mitandaoni.

Hii ilidhihirika wakati mbunge wa Ghana hivi majuzi aliposimama kuhutubia bunge akiwataka wenzake kuwa makini zaidi wasije wakaibua hasira ya umma kama inavyoonekana nchini Kenya.

“Wananchi wa Kenya wanawapiga wabunge kwa kupitisha sheria mbovu, Mheshimiwa Spika, ni jambo zito, niliona wabunge wenzangu wakipigwa kichapo cha mbwa,” alisema.

Huku kukiwa na manung'uniko na vicheko, mbunge huyo aliendelea kuonya kuwa si jambo la mzaha.

Matukio ya vijana nchini Kenya wakivamia majengo ya bunge na kuteketeza sehemu za ukumbi wa kaunti, huku wakiwatuma wabunge wao kutawanyika kwa hofu huenda yalipelekea hali halisi ya mwamko si kwa tabaka tawala pekee bali wananchi wa kawaida pia.

Baadhi ya nchi za Afrika zinatumia nguvu kupita kiasi kukabiliana na maandamano / Picha : Reuters 

Tangu kuanza kwa maandamano nchini Kenya mwishoni mwa mwezi Juni, mitandao ya kijamii ilijaa ujumbe wa kutia moyo na wakati mwingine wa tahadhari kutoka kwa nchi jirani huku baadhi wakihoji ni kwa nini vijana katika nchi zao hawawezi kusimama kwa ujasiri kama Wakenya.

Wachanganuzi wanaonya kuwa iwapo kuna lolote, maandamano ya Kenya yanafaa kuwa mwamko kwa watu walio mamlakani.

‘’Watu wengi baada ya kuchaguliwa wanaonekana kusahau walichaguliwa kuhudumu na si kutawala,’’ anasema Ade Daramy, mchambuzi wa masuala ya kisiasa na mhariri wa habari kutoka Sierra Leone. ‘’Si jambo la Wakenya tu, wananchi wanataka kusikilizwa na kushauriwa. Si kufanya maamuzi makubwa peke yako,’’ Ade anaiambia TRT Afrika.

Jirani wa Kenya, Uganda, pia ameona vijana wakikusanyika mtandaoni ili kutoa wito wa mabadiliko na kuheshimiwa kwa utawala wa sheria, japo mtandaoni.

Vijana wa huko wamekuwa wakilalamika kwamba kinyume na wenzao wa Kenya, wanaogopa zaidi aina ya nguvu inayotumiwa kuwaondoa waandamanaji. Wachambuzi wanahofia kwamba nchi ambazo hazisikilizi watu wao zinajiweka katika mazingira ya kushindwa.

‘’Mfano mzuri, sio mbali sana, tuliona kilichotokea Sudan. Wananchi walianza kulalamika lakini serikali ikawapuuza. Walipoingia mitaani, walikabiliwa na nguvu kupita kiasi, na walilipiza kisasi na yote yakaongezeka kwa uasi na vita tunavyoviona sasa,’’ anasema Wamoto Wabete, mkuu wa wilaya mstaafu nchini Uganda na mtaalamu wa masuala ya utawala.

‘’Kuna somo kwa pande mbili hapa. Kwamba serikali zinapaswa kujifunza kuwa zinafaa kuwatumikia watu wao lakini pia wananchi wanapaswa kuelewa kuwa serikali ilichaguliwa kihalali kuwawakilisha na pia waruhusiwe kufanya kazi zao ndani ya mfumo wa kisheria,’’ Wamoto anaiambia TRT Afrika.

Lakini iwapo mapinduzi ya Gen Z yanaweza kupita zaidi ya Kenya ni suala tofauti kabisa.

Mchambuzi Ade anasema licha ya kuonyesha mshikamano na kwa kiasi fulani wivu kwa wenzao wa Kenya, vijana wanahitaji kufikiria kwa tahadhari, kwa sababu kinachofanya kazi nchini Kenya huenda kisifanye kazi kwa wengine nje ya Kenya.

‘’Tunahitaji kuwa waangalifu sana tunapolinganisha,’’ anaiambia TRT Afrika. Hali nchini Kenya ni tofauti na zile za Senegal. Afrika sio nchi moja. Masuala huenda yanafanana lakini hali katika Afrika Mashariki ni tofauti na Afrika Magharibi,’’ anaongeza.

Mashaka hayo ni kati ya mtindo wa utawala, kiwango cha uhuru wa kujieleza na hata namna polisi wanavyotumiwa. Baadhi ya nchi zinatumia nguvu zaidi kuliko vyengine.

Wachambuzi wanasema ni wakati wa vijana kujihusisha zaidi katika siasa za nchi yao. / Picha : Reuters 

‘’Tuliona nchini Senegal, vijana walijaribu kuandamana dhidi ya utawala, lakini walikabiliwa na nguvu nyingi ambazo zilisababisha vifo vya watu wengi,’’ Ade anasema. ‘’Lakini waliamua kutumia kura kuuondoa utawala ule ule na ulifanya kazi,’’ anaeleza.

Unapochambua na kutenganisha kelele na msisimko, utakutana na baadhi ya wanamtandao wanaowaita wavulana na wasichana hawa wachanga kuhamishia nguvu hizi kwenye sanduku la kura.

Mara nyingi wale wanaolalamika sana kuhusu serikali wameshutumiwa kwa kutoshiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi. Kifupi hawapigi kura.

"Inakufanya ujiulize, ni msukumo wa kufanya maandamano tu au? Wakati mwingine kile tunachokiona si dhihirisho la kweli la nia yao katika siasa,’’ anasema Ade. ‘’Waandamanaji wengi wana hasira na sauti lakini mwisho wao ni hapo Tiktok na twitter,’’ Ade anaiambia TRT Afrika.

Ade anasema ni wakati wa vijana kujihusisha zaidi katika siasa za nchi yao.

‘’Ningeamini wanavutiwa na siasa zao ikiwa ushahidi na taarifa zipo kusaidia. Ikiwa watu walijiunga na tawi la vijana la vyama vya siasa au hata kuanzisha vyama vyao, wangeleta mabadiliko,’’ anaiambia TRT Afrika.

Tangu kuanza kwa maandamano ya kupinga ushuru nchini Kenya, Juni 25, rais amekubali baadhi ya matakwa ya Gen Z.

Hata hivyo vijana wameendelea kuandamana wakiongeza madai zaidi kwenye orodha yao ambayo wachambuzi wanaonya kuwa yanaweza kupotosha mwelekeo wao.

Baadhi ya vijana kutoka nchi mbali mbali za Afrika wamekuwa wakishinikiza vijana wenzao kuiga mfano wa Kenya na kuandaa maandamano dhidi ya hali ngumu ya maisha/ Picha: Reuters

‘’Ni vyema serikali ikasikiliza wananchi na kuwapa wanachotaka. Lakini waandamanaji pia wanapaswa kujua wakati inatosha. Wasije wakazidisha maji unga. Sio lazima kusukuma maandamano yako kupita kiasi, kwa sababu unapoteza uaminifu,’’ Wamoto anasema.

Vijana wengi kote barani Afrika walishangilia walipoona maandamano ya Wakenya yakizaa matunda. Wengine walikwenda mbali zaidi kuomba maandamano kama hayo katika nchi zao.

Lakini kama Ade anavyoonya, hii inapaswa kuwa chaguo ya mwisho wakati diplomasia itashindwa.

"Ni rahisi kusema kuliko kutenda. Mimi natoka Sierra Leone na nimeona upande mbaya wa maandamano. Ninatahadharisha watu kutotamani mambo haya. Vurugu daima huzaa vurugu,’’ anaiambia TRT Afrika.

TRT Afrika