Ethiopia imezima shambulio la kundi la waasi wa Al-Shabaab / Photo: Reuters

Ethiopia inasema imezima shambulio la kundi la waasi la Al-Shabaab kwenye mji ulio kwenye mpaka wake na Somalia.

Wizara ya Mambo ya nje ya Ethiopia ilisema jeshi la taifa lilifanikiwa kuzuia jaribio ya "kufanya uharibifu" katika mji wa mpakani wa Ethiopia na Somalia wa Dollo.

‘’Jeshi la taifa, iliwazuia washambuliaji wa kujitoa mhanga na kuharibu silaha ambazo zingetumiwa na kundi hilo la kigaidi,’’ ilisema wizara hiyo katika taarifa fupi kwenye mtandao wa kijamii siku ya Jumatano.

Mji wa Dollo nchini Ethiopia iko chini ya kilomita tatu (maili 2) kutoka kwa mji wa Somalia unaoitwa, Doolow.

Waasi wa Al-Shabaab, wanaohusishwa na kundi la waasi la Al-Qaeda, wamekuwa wakiendesha uasi dhidi ya serikali kuu ya Somalia kwa takriban miaka 15.

Kundi hilo lilidai kupitia njia zake za mawasiliano kwamba lilifanya mashambulizi mawili ya kujitoa mhanga katika kambi ya kijeshi ya Ethiopia kwenye mpaka wa Somalia. Hii ni kwa mujibu wa shirika la ufuatiliaji la Marekani linaloitwa SITE, shirika la habari la AFP linaripoti.

Kundi hilo lilifurushwa kutoka Mogadishu mwaka 2011 na kikosi cha Umoja wa Afrika, lakini bado linadhibiti maeneo mengi ya mashambani na linaendelea kufanya mashambulizi mabaya dhidi ya malengo ya kiraia, kisiasa na kijeshi.

TRT Afrika na mashirika ya habari