Athari ya mzozo kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran kwa Mazingira
MAZINGIRA
2 dk kusoma
Athari ya mzozo kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran kwa MazingiraMakadirio ya wataalam ya athari za mzozo huo yanaonyesha kuwa uzalishaji wa hewa chafu za kaboni unaotokana na mzozo ulifikia zaidi ya tani milioni 5 katika wiki mbili za kwanza za vita
Meli kadhaa zimezamishwa baharini na hapo kuathiri maisha ya viumbe wa majini / Reuters
8 Aprili 2026

Mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran yaliyoanza Februari 28, na Iran kuanza kulipiza kisasi kwa kuishambulia Israel na baadhi ya miundombinu ya Marekani iliyopo katika mataifa jirani ya nchi za Ghuba, yamesababisha na yanaendelea kusababisha madhara makubwa kwa mazingira.

Kufuatia mapigano hayo, jeshi la wanamaji la Iran limepoteza zaidi ya meli 43, ambazo zinaripotiwa kuharibiwa au kuzamishwa.

Kando na uchafu huu mkubwa ambao utabaki baharini kwa karne na karne, bado kuna athari ya mafuta ambayo yamemwagika baharini baada ya meli za mafuta kushambuliwa hivyo kutishia viumbe hali vya baharini.

Kando na hayo mashambulizi yaliyolenga miundombinu ya bandari huko Abu Dhabi, Dubai, Jebel Ali na Manama yaliharibu meli na vifaa vya bandari, na kueneza uchafu wa mafuta katika maji yanayozunguka.

Kulipuliwa kwa viwanda vya mafuta kunapelekea kemikali kuingia hewani na wataalamu wanaonya zinaweza kusababisha mvua ya asidi, na uwepo wa kemikali hizo unaweza kuongeza hatari ya magonjwa ya saratani, kuwashwa kwa ngozi na macho, na magonjwa ya moyo na mishipa.

Hii imeibua hali ya wasiwasi, kwa sababu iwapo uchafu huu utaingia kwenye vyanzo vya maji, basi athari za muda mfupi na mrefu zitashuhudiwa.

Utoaji wa kaboni pia ni hatari.

Pia kaboni dioksidi na gesi nyengine chafu kwenye anga hewa, zimeongeka kutokana na uharibifu wa majengo, milipuko katika vituo vya mafuta, mafuta yanayotumika katika mapigano na shughuli za usaidizi, kaboni iliyopachikwa kwenye vifaa vya kijeshi na utoaji wa hewa chafu kutoka katika makombora na droni.

Makadirio ya wataalam ya athari za mzozo huo yanaonyesha kuwa uzalishaji wa hewa chafu za kaboni unaotokana na mzozo ulifikia zaidi ya tani milioni 5 katika wiki mbili za kwanza za vita, na kuzidi uzalishaji wa kila mwaka wa Iceland.

Mzozo huo pia unatishia usalama wa maji kwa nchi za ghuba.

Nchi za Mashariki ya Kati zinakabiliwa na hali kame na uhaba wa maji mara kwa mara, mara nyingi hutegemea miundombinu ya kuondoa chumvi kutoka maji ya baharini na kuyageuza kuwa maji safi na salama kwa matumizi ya binadamu.

Bila teknolojia kama hiyo, ambayo huondoa chumvi, takriban watu milioni 100 katika Mashariki ya Kati hawangeweza kupata maji ya kunywa mara kwa mara.

Kuna takriban mimea elfu tano ya kuondoa chumvi katika Mashariki ya Kati, zaidi ya mia nne ambayo iko katika Ghuba.

Mitambo ya kuondoa chumvi nchini Kuwait na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) ilikuwa ni sehemu ya miundombinu iliyoshambuliwa.

Kadiri mzozo unavyoendelea ndivyo mazingira yanavyozidi kuwa hatarini.

CHANZO:TRT Swahili