Serikali ya Kenya imezindua bima ya lazima kwa watalii wanaoingia nchini humo.
Mpango huo, utawalazimu watalii wote kuwa na bima ya afya yenye kiwango cha chini cha karibu Dola 50,000 kulingana na tangazo lililochapishwa kwenye Gazeti Rasmi la Serikali la Julai 30, 2026 na kutiwa sahihi na Waziri wa Afya, Aden Duale.
Mpangilio huo, unahusisha gharama za matibabu ya walau Dola 20,000, Dola 25,000 kwa ajili ya uokoaji wa dharura, Dola 5,000 za kurudishwa nyumbani, Dola 1,000 kwa ajili ya huduma za afya ya akili na Dola 300 kwa ajili ya madawa.
Kulingana na serikali, hatua hiyo inalenga kuhakikisha watalii wanapata huduma wanapokumbwa na dharura za kiafya.
Hata hivyo, uamuzi huwa umekoselewa vikali na baadhi ya wadau wa utalii nchini humo, wakidai kuwa utaongeza gharama za kuitembela Kenya kwa shughuli za kitalii.
Miaka miwili iliyopita, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), ilianzisha bima kwa wageni watalii, yenye thamani ya Dola 44.
Kulingana na Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Saada Mkuya Salum, mpango huo unalenga kuongeza kasi ya idadi ya watalii kufika Zanzibar na serikali kupata mapato yatokanayo na sekta ya utalii.



















