Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, amesema ametumia hotuba yake ya 16 mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UN) kuhimiza wito wa kuwepo kwa mfumo wa kimataifa wenye haki zaidi, huku akisisitiza tena msimamo wa Uturuki wa kuiunga mkono Palestina.
“Tutaendelea kusema kwa ujasiri kile tunachoamini kuwa ni sahihi na kusema ukweli,” Erdogan alisema baada ya kikao cha Baraza la Mawaziri kilichofanyika Ankara siku ya Jumatatu.
Akieleza ushiriki wake katika Mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, Erdogan alisema aliwasilisha mfumo wa hoja wenye vipengele vitano kwa ajili ya kuanzishwa kwa utaratibu mpya wa kimataifa unaozingatia zaidi haki, uwakilishi mpana zaidi, uaminifu na ustawi.
“Hatutarejea nyuma”
Erdogan alisema ugaidi unaofanywa na Israel huko Gaza na Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kinaendelea kuwa miongoni mwa masuala yanayopewa kipaumbele katika ajenda ya kimataifa ya Uturuki.
Alikosoa kutokuwepo kwa Rais wa Palestina, Mahmoud Abbas, katika Mkutano Mkuu wa UN, akisema kuwa vikwazo vya viza vilimzuia kuhudhuria mkutano huo ana kwa ana.
“Wakati wahalifu wa kivita ambao maneno yao yananuka damu walipopata nafasi kwenye jukwaa la UN kueneza uongo wao, ukweli kwamba Rais Abbas hakuweza kuwepo ni hali ya aibu kwa ubinadamu,” Erdogan alisema.
Alisema Uturuki itaendelea kuwaunga mkono Wapalestina pamoja na Walebanon walioathiriwa na migogoro hiyo.
“Hatutaachana kamwe na msimamo wetu hadi wale wanaofanya uhalifu dhidi ya ubinadamu, wale ambao wamemwaga damu ya ndugu na dada zetu 74,000 huko Gaza, na wale ambao wameeneza ugaidi katika eneo letu kutoka Lebanon hadi Syria wawajibishwe mbele ya sheria,” alisema.
Pia alieleza misimamo ya Uturuki kuhusu hali ya Gaza na Ukingo wa Magharibi unaokaliwa, vita vya Urusi na Ukraine, pamoja na mvutano unaohusisha Iran.
Diplomasia na ushirikiano wa kiuchumi
Erdogan alisema alifanya mikutano ya pande mbili na wakuu wa nchi na serikali 17 wakati wa ziara yake mjini New York. Pia alihudhuria mkutano uliowakutanisha Marekani na nchi za Baraza la Ushirikiano la Ghuba (GCC) kwa mwaliko wa Trump.
“Kwa mwaliko wa Bw. Trump, nilihudhuria mkutano uliowakutanisha Marekani na nchi za Baraza la Ushirikiano la Ghuba, ambapo nilieleza maoni yetu kuhusu kurejesha amani na utulivu katika eneo hili,” alisema.
Aidha, Erdogan alisema alikutana na wawakilishi wa wafanyabiashara wa Marekani kujadili fursa za uwekezaji nchini Uturuki, na pia alishiriki katika programu zilizowakutanisha jumuiya za Uturuki, Marekani na Waislamu.
Erdogan alisisitiza umuhimu wa Jumba la Uturuki mjini New York kama kitovu cha shughuli za kidiplomasia. Pia alizungumza kuhusu ushiriki wake katika hafla ya kufunga Maonesho ya 21 ya Kimataifa ya Biashara ya MUSIAD EXPO pamoja na Jukwaa la 29 la Kimataifa la Biashara, yaliyofanyika Septemba 26.
Alisema mawasiliano na mikutano iliyofanyika wakati wa Mkutano Mkuu wa UN yatakuwa na manufaa kwa Uturuki na kwa jamii zilizoathiriwa na migogoro. Pia alieleza matumaini kwamba mikutano hiyo itazaa ushirikianompya.




























