Mfanyabishara kutoka Nigeria, Aliko Dangote, ametangaza kuwa kampuni yake imenunua asilimia 25 ya hisa za Kampuni ya Kenya Pipeline inayosambaza mafuta.
Dangote amesema hayo siku ya Jumatano wakati wa Mkutano wa Afrika ulioandaliwa na gazeti la Financial Times jijini London, Uingereza.
Mwezi uliopita, mfanyabiashara huyo alizindua rasmi ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta katika bandari ya Lamu nchini Kenya. Kiwanda hicho kinatarajiwa kuwa na uwezo wa kusafisha mapipa 700,000 ya mafuta kwa siku.
Dangote, ambaye ndiye tajiri mkubwa zaidi barani Afrika, tayari anamiliki na kuendesha kiwanda cha kusafisha mafuta chenye uwezo sawa na huo karibu na jiji la Lagos nchini Nigeria. Himaya yake ya biashara pia inajumuisha viwanda vya mbolea, saruji na sukari, pamoja na uwekezaji katika sekta nyingine.
Kenya yaongeza juhudi za kukuza mapato ya serikali
Katika hotuba yake Jumanne, Rais wa Kenya, William Ruto, alisema kuwa wawekezaji binafsi wamepata hisa za asilimia 25 katika mtandao wa mabomba ya mafuta nchini humo, ambazo awali zilikuwa zinamilikiwa na taasisi za umma. Hata hivyo, hakuwataja wawekezaji hao.
Mapema mwaka huu, serikali ya Kenya iliuza hisa za asilimia 65 katika Kampuni ya Kenya ya Pipeline kupitia mfumo wa mashirika ya umma yanayoingia sokoni kwa mara ya kwanza (IPO).
Hatua hiyo ilikuwa sehemu ya juhudi za serikali kuongeza mapato yake, wakati ambapo uwezo wake wa kifedha wa kugharamia matumizi na miradi ya umma ikipitia changamoto.






















