Serikali ya Uganda inapanga kuweka uzio wa umeme kuzunguka maeneo ya makazi ndani ya wilaya zinazopakana na maeneo ya hifadhi.
Mpango huo, unalenga kupambana na changamoto ya migongano kati ya binadamu na wanyamapori, kulingana na waziri wa utalii wa nchi hiyo, Susan Nakawuki.
Akizungumza bungeni, waziri huyo alisema kuwa, uzio huo wa umeme utajengwa kuzunguka hifadhi ya taifa ya Malkia Elizabeth, iliyo kati ya wilaya za Rukungiri na Mitooma.
Kauli ya waziri huyo, inafuatia hoja iliyoibuliwa na mbunge wa Nyabushozi, Wilson Kajwengye, ambaye alidai kuwa wanyamapori katika hifadhi ya Ziwa Mburo, wamekuwa wakiharibu mazao, vyanzo vya maji na kusababisha vifo vya binadamu.
Mbunge huyo alibainisha kuwa, kumekuwa na athari kubwa za wanyama waharibu katika eneo lake.
“Watu wa maeneo haya wamekosa chakula kutokana na wanyamapori waharibu. Naomba serikali iingilie kati suala hili,” alisema Kajwengye.
Migogoro kati ya wanyamapori na binadamu ni mapambano yanayotokea pale ambapo mahitaji ya wanyama yanapogongana na shughuli au maisha ya watu.
Migogoro hii husababisha vifo, uharibifu wa mazao, na uharibifu wa mali, na mara nyingi huchochewa na upanuzi wa makazi na kilimo katika shoroba asili za wanyama.















