| Swahili
AFRIKA
3 dk kusoma
Botswana yakosolewa kwa kuidhinisha kuuawa kwa tembo 23 kusherehekea Siku ya Uhuru
Mamlaka zilisema kuwa nyama ya tembo hao itatolewa nyama kwa jamii zenye uhitaji vijijini, huku nchi hiyo ikiadhimisha miaka 60 tangu kupata uhuru kutoka kwa Uingereza.
Botswana yakosolewa kwa kuidhinisha kuuawa kwa tembo 23 kusherehekea Siku ya Uhuru
Botswana inakadiriwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya tembo duniani. / / AA

Serikali ya Botswana imeidhinisha kuuawa kwa tembo 23 kwa ajili ya sherehe za Siku ya Uhuru wa nchi hiyo wiki hii, hatua ambayo imekosolewa na wanaharakati wa kuhifadhi mazingira. Hatua hiyo pia imekosolewa na aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Ian Khama.

Leseni za kuwinda tembo hao zilitolewa katika wilaya mbalimbali nchini humo, huku kila wilaya ikitengewa sehemu na jumla ya idadi ya tembo walioruhusiwa kuwinda. Kwa mujibu wa mamlaka, nyama ya tembo hao itatolewa kwa jamii maskini za vijijini. Serikali ilitoa kauli hiyo Ijumaa ikitetea uamuzi huo.

Ingawa tembo wa savanna wa Afrika wameorodheshwa kama wanyama walio katika hatari ya kutoweka na Muungano wa Kimataifa wa Uhifadhi wa Mazingira (IUCN), Botswana, ambayo ni nchi ya kusini mwa Afrika, ina idadi kubwa ya tembo inayokadiriwa kufikia takribani 130,000, idadi kubwa kuliko nchi nyingine yoyote duniani.

Mfumo wa Botswana wa kuweka idadi maalumu ya tembo wanaoruhusiwa kuwindwa kila mwaka umewahi kukosolewa hapo awali. Hata hivyo, serikali imekuwa ikiutetea kwa hoja kwamba ni muhimu katika kudhibiti ongezeko la idadi ya tembo na pia kupunguza migogoro kati ya binadamu na tembo.

Marufuku ya uwindaji yaondolewa

Botswana iliondoa marufuku ya kuwinda tembo mwaka 2019, hasa kutokana na kuongezeka kwa idadi yao. Katika miaka ya hivi karibuni, serikali imekuwa ikiweka viwango vya kila mwaka vinavyoruhusu kuwindwa kwa tembo kati ya 200 na zaidi ya 400, kutegemea mwaka husika.

Wiki hii, serikali pia iliidhinisha kuuawa kwa makumi ya wanyama aina ya swala kama sehemu ya mpango huo. Hatua hiyo ilikuja wakati Botswana ikiadhimisha miaka 60 ya uhuru wake kutoka kwa Uingereza siku ya Jumatano. 

Jumuiya ya Kulinda Tembo wa Botswana ilikosoa uamuzi huo wa kuwaua tembo, ikisema ni wa kutowajibika na unaweza kusababisha makundi ya tembo kuwa wakali zaidi dhidi ya watu wanaoishi karibu nao.

“Tembo mmoja anapopigwa risasi, wengine huwa na tabia ya kujilinda,” ilisema jumuiya hiyo.

Migogoro kati ya binadamu na wanyamapori

Migogoro kati ya binadamu na wanyamapori ni tatizo kubwa katika nchi nyingi za Afrika. Nchi nyingine, zikiwemo jirani yake Afrika Kusini, pia huweka viwango vya kila mwaka vya idadi ya tembo wanaoruhusiwa kuwindwa.

Uwindaji wa tembo uliofanyika wiki hii ulitetewa na Dimakatso Ntshebe, naibu mkurugenzi katika Idara ya Wanyamapori na Hifadhi za Taifa ya Botswana.

“Uhifadhi wa wanyamapori lazima utoe manufaa ya maana kwa jamii zinazoishi pamoja na wanyamapori na zinazochangia katika kuwalinda,” alisema Ijumaa.

Hata hivyo, Ian Khama, ambaye alikuwa rais wa Botswana kuanzia mwaka 2008 hadi 2018 na ambaye sasa anashikilia nafasi ya kimila ya uongozi kama chifu wa eneo, alisema hakubaliani na uamuzi huo. Alisema hatua hiyo inaweza kujenga “matarajio” kwamba tembo watauawa kila mara kunapokuwa na matukio ya kitaifa yajayo.

 

CHANZO:AP