Misri imekanusha kuingilia mambo ya ndani ya nchi yoyote, kufuatia shutuma kutoka Ethiopia kwamba Misri inaunga mkono makundi yenye silaha katika eneo la kaskazini mwa nchi hiyo.
“Misingi ya sera ya mambo ya nje ya Misri inajengwa juu ya kanuni thabiti, kwanza ikiwa ni kuheshimu mamlaka ya nchi, umoja wake na uhuru wa mipaka yake ya kitaifa, pamoja na kutokuingilia mambo ya ndani ya nchi nyingine,” alisema msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Nader Zaki, katika ujumbe aliouchapisha Jumatatu jioni kwenye mtandao wa kijamii wa X.
“Kwa msingi huo, madai yoyote yanayotilia shaka dhamira ya Misri katika kuzingatia kanuni hizi zilizokita mizizi ni batili na hayana msingi,” aliongeza.
Zaki hakutaja nchi au upande uliotoa madai hayo.
Mapigano makali yaanza tena
Awali, Kamanda wa Jeshi la Ethiopia, Field Marshal Birhanu Jula, aliishutumu Sudan, Misri na wahusika wengine kwa kuunga mkono makundi yenye silaha yanayopambana na majeshi ya Ethiopia kaskazini mwa nchi hiyo.
Shutuma hizo zilitolewa baada ya mapigano makali kuanza tena kati ya waasi wa Tigray People’s Liberation Front (TPLF) na serikali ya shirikisho.
Ethiopia ilikumbwa na vita vya umwagaji damu kuanzia mwaka 2020 hadi 2022 kati ya majeshi ya serikali na waasi wa TPLF. Kwa mujibu wa Umoja wa Afrika, vita hivyo vilisababisha vifo vya watu takribani watu 600,000, kabla ya pande hizo mbili kusaini Mkataba wa Pretoria, uliolenga kukomesha mzozo huo.





















