Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, amezitaka nchi zilizoendelea kuchukua jukumu kubwa zaidi katika kupunguza hewa chafuzi na kugharamia hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, akisisitiza kuwa nchi hizo zinapaswa kuwajibika pakubwa kutokana na mchango yake katika matumizi ya rasilimali ya hewa chafuzi duniani.
Akizungumza siku ya Alhamisi katika Jukwaa la Biashara la COP31 lililofanyika Antalya, kusini mwa Uturuki, Erdogan amesema ukubwa wa athari za mabadiliko ya tabianchi unahitaji hatua za haraka na za dhati kutoka kwa mataifa yote duniani.
Amesisitiza kuwa nchi zilizoendelea, ambazo kwa kiasi kikubwa zimeshatumia sehemu kubwa ya kiwango cha hewa ukaa duniani, zinapaswa kuongeza juhudi za kupunguza uzalishaji wa hewa chafuzi na kutoa ufadhili na kusaidia kukabiliana na changamoto hiyo.
"Nchi zilizoendelea ambazo zimetumia sehemu kubwa ya bajeti ya kimataifa ya hewa chafuzi zinapaswa kuwajibika pakubwa zaidi katika kupunguza uzalishaji wa hewa chafuzi na kutoa ufadhili," alisema Erdogan.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kulinda haki ya nchi zinazoendelea kujiimarisha kiuchumi na kijamii, huku akitaka jamii zinazokumbwa zaidi na athari za mabadiliko ya tabianchi kupewa msaada wa kutosha.
Erdogan ameonya dhidi ya mataifa kuweka mbele maslahi yao binafsi na kupuuza wajibu wa pamoja katika kukabiliana na changamoto za mazingira. Amesema mtazamo huo unaweza kuongeza matatizo na kusababisha majanga makubwa zaidi.
"Ikiwa tutachukua msimamo wa kusema kwamba 'kila mtu ajali mambo yake mwenyewe', tutafungua mlango wa changamoto kubwa zaidi na majanga yenye madhara makubwa zaidi," alionya.
Rais huyo pia amesema kuwa maamuzi yaliyofanywa katika miaka ya nyuma, kwa kutanguliza maslahi ya kiuchumi na kupuuza uhifadhi wa mazingira, yanaanza kuonyesha madhara yake. Alisema dunia inapaswa kujifunza kutokana na makosa hayo badala ya kuyarejelea.
"Makosa yaliyofanywa miaka 50 au 100 iliyopita sasa yanaanza kujitokeza moja baada ya jingine. Tukirudia makosa hayo leo na kutoa kipaumbele kwa uchumi zaidi ya mazingira, watoto wetu ndio watakaolipa gharama yake," alisema.
Erdogan athibitisha kuendelea kuwekeza katika nishati mbadala
Akizungumzia hatua zinazochukuliwa na Uturuki, Erdogan amesema nchi hiyo inaendelea kutekeleza mkakati wake wa maendeleo endelevu yanayojali mazingira kwa kufanya mageuzi katika sekta mbalimbali, zikiwemo nishati, viwanda, usafirishaji, kilimo na ujenzi.
Amebainisha kuwa juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi haziwezi kufanikiwa kwa kutegemea serikali pekee, bali zinahitaji pia ushiriki na uwajibikaji mkubwa zaidi kutoka kwa sekta binafsi na wafanyabiashara.
Erdogan amesema Uturuki inalenga kuimarisha ushindani wa viwanda vyake huku ikiendelea kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Ameahidi kuwa serikali itaendelea kuunga mkono uwekezaji katika vyanzo vya nishati mbadala, hususan nishati ya upepo, jua na maji.
Kuhusu changamoto ya kupanda kwa bei za nishati, Erdogan alikiri kuwa Uturuki nayo inaathiriwa na hali hiyo, kama zilivyo nchi nyingine duniani. Hata hivyo, alisisitiza kuwa serikali yake haitaachana na malengo ya kukuza uchumi, kuendeleza nchi na kuwekeza katika miradi inayolenga kuboresha ustawi wa wananchi.
Akigusia hali ya usalama na maendeleo ya kikanda, Erdogan alisema Uturuki imeendelea kujidhihirisha kama nchi yenye utulivu na usalama, huku imani ya wawekezaji wa kimataifa na taasisi mbalimbali za kimataifa ikiendelea kuimarika.
"Tunaendelea kuilinda nchi yetu dhidi ya migogoro, huku tukifanya kazi kwa dhati kuhakikisha amani na utulivu vinapatikana katika eneo letu," alisema.
Aliongeza kuwa: "Uturuki ni nchi yenye uwezo wa kubadilisha ndoto zake kuwa malengo, na malengo hayo kuyatekeleza hadi kuwa uhalisia."




















