Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan amekutana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, pembezoni mwa mkutano wa COP31 unaofanyika mjini Antalya, nchini Uturuki, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ikulu ya Uturuki.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa Jumanne, viongozi hao wawili walijadili masuala mbalimbali ya kikanda na kimataifa, yakiwemo mvutano kati ya Iran na Marekani, vita nchini Ukraine, pamoja na yanayojiri katika Ukanda wa Gaza, Cyprus na Libya.
Katika mazungumzo hayo, Erdogan alisema Uturuki imefurahishwa na jukumu la kuongoza mkutano wa COP31 na kwamba maandalizi ya kuhakikisha mkutano huo unafanikiwa yamekamilika.
Alieleza matumaini kuwa mkutano huo, unaoandaliwa na Uturuki katika jiji la Antalya lililopo kusini mwa nchi hiyo, utakuwa mwanzo mpya katika juhudi za kukabiliana na changamoto zinazohusiana na mabadiliko ya tabianchi.
Akizungumzia mvutano wa kikanda, Erdogan amesema Uturuki inaendelea kushirikiana na nchi nyingine za eneo hilo katika juhudi za kupunguza mvutano kati ya Iran na Marekani.
Alisisitiza kuwa Uturuki imejizatiti kusaidia kutatua migogoro kupitia mazungumzo na diplomasia, kwa mujibu wa taarifa hiyo.
Kuhusu vita vinavyoendelea kati ya Urusi na Ukraine, Erdogan amesema Uturuki inaendelea na juhudi za kumaliza vita hivyo na iko tayari kusaidia kuanzishwa kwa mchakato mpya wa mazungumzo kati ya pande zinazohusika.
Viongozi hao pia walijadili yanayojiri katika Ukanda wa Gaza, Cyprus na Libya, taarifa hiyo imesema.
Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Mke wa Rais wa Uturuki, Emine Erdogan; Waziri wa Mambo ya Nje, Hakan Fidan; Waziri wa Mazingira, Miji na Mabadiliko ya Tabianchi, Murat Kurum; Waziri wa Afya, Kemal Memişoğlu; pamoja na Mkuu wa Mawasiliano wa Uturuki, Burhanettin Duran.
Wengine walioshiriki ni pamoja na Makamu Mwenyekiti na Msemaji wa Chama AK Party, Ömer Çelik, pamoja na Rais wa Taasisi ya Kutokuwepo kwa Taka (Zero Waste), Samed Ağırbaş.





















