| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
Erdogan wa Uturuki asisitiza 'makubaliano yaheshimiwe' kuhusu Gaza, alaumu ugaidi wa walowezi Israel
Rais wa Uturuki anasema yanayojiri katika kanda yanaonesha kuwa mifumo "inapeperusha bendera nyeupe kujisalimisha".
Erdogan wa Uturuki asisitiza 'makubaliano yaheshimiwe' kuhusu Gaza, alaumu ugaidi wa walowezi Israel
Rais wa Uturuki anasema yanayojiri katika kanda yanaonesha mifumo 'inapeperusha bendera nyeupe ya kujisalimisha.' /Picha: AA

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan anasema kuwa matukio ya hivi karibuni katika kanda yanaonesha kuwa mifumo ya kimataifa “yanapeperusha bendera nyeupe ya kujisalimisha,” kushtumu taasisi za dunia kwa kutokuchukua hatua huku vurugu za Israel zikiendelea Gaza na Ukingo wa Magharibi uliokaliwa.

Erdogan siku ya Ijumaa alionya kuwa mfumo wa kimataifa umeshindwa kusimamia usalama na amani.

Akizungumza katika hafla rasmi ya ufunguzi ya kongamano la TRT World Forum 2026 Ukumbi wa Mkutano wa Istanbul, Erdogan alisema:

“Ugaidi wa walowezi, ambao unataka kuwaondoa Wapalestina kutoka kwenye ardhi za mababu zao kwa lazima, unaendelea kwa ukatili kila siku huku dunia ya kisasa ikijifanya kutoona hilo.”

Makubaliano yaheshimiwe

Taasisi za kimataifa zilizo na majukumu ya kuhakikisha amani, usalama na uthabiti kwa mara nyingine “zimekaa pembeni” huku ukatili ukiendelezwa Gaza, kama ilivyokuwa Rwanda, Srebrenica na maeneo mengine mengi, alieleza.

“Kwa bahati mbaya, Mpango wa Amani wa Gaza, ambao tulisaidia kuleta upatanishi, hautekelezwi,” Erdogan alieleza.

Akisisitiza kuhusu msingi wa "pacta sunt
servanda" au ‘‘makubaliano yaheshimiwe’’, ambayo yanasisitiza uhusiano wa kimataifa, haiheshimiwi, Erdogan alisema, "Kila mtu lazima aelewe kuwa hakuna tatizo ambalo linaweza kutatuliwa kwa njia hii.”

Rais wa Uturuki anasema misingi ambayo mfumo wa kimataifa umejengwa “leo hii inavunjwa.”

Erdogan alieleza kuwa mizozo ilioko kwa sasa duniani haiwezi kutatuliwa kwa mitazamo iliopitwa na wakati.

“Hatuwezi kutatua matatizo ya sasa kwa njia ya kizamani,” alisema.

Dunia Bila Mwelekeo

Katika hotuba ya ufunguzi, kwa kongamano la TRT World Forum, ambalo kauli mbiu yake ya mwaka huu ni “Dunia Bila Mwelekeo", Erdogan aliupongeza na kuushukuru uongozi wa TRT kwa kuandaa jukwaa la mwaka huu, akilitaja kuwa kitambulisho kikuu cha shirika hilo la habari.

Alisema kuwa TRT kwa miaka 60 imekuwa ikitangaza kwa kuzingatia misingi thabiti ya utangazaji kwa majukwaa yote ya kawaida na ya kidijitali.

Alieleza matumaini yake kuwa majadiliano ya jukwaa hilo “yatafungua upeo” na kwamba ujumbe unaotolewa utasaidia katika usalama na amani duniani, hasa katika maeneo ambayo watu wanateswa na kunyanyaswa.