Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan atatembelea Jamhuri ya Uturuki ya Kupro Kaskazini (TRNC) siku ya Ijumaa, kulingana na vyanzo vya kidiplomasia.
Wakati wa ziara hii, Fidan anatarajiwa kulakiwa na Rais wa TRNC Tufan Erhurman na Waziri Mkuu Unal Ustel.
Pia atakutana na Waziri wa Mambo ya Nje Tahsin Ertugruloglu.
Mikutano hiyo itaangazia masuala ya mataifa mawili na yanayojiri kuhusu suala la Kupro, vyanzo hivyo vilisema.
Uturuki inaendelea na juhudi zake, katika nafasi yake kama mdhamini wa taifa, kuhakikisha kuna usalama, maendeleo na mafanikio ya watu wa Uturuki ya Kupro, wakati ikiendelea kuunga mkono haki zao kuishi kwa amani na kwa mafanikio katika kisiwa hicho kama washirika sawa, vyanzo hivyo vilisema.
Uturuki inasisitiza kuwa suluhu ya uhakika kwa suala la Kupro ni msingi wa ushirikiano wa mataifa mawili katika kisiwa hicho na hadhi ya usawa kimataifa kwa Waturuki wa Kupro, ambayo inaamini ni haki yao ya kimsingi, inayotakiwa kutambuliwa na jamii ya kimataifa.
Uturuki inasema kuwa suala la Kupro bado halijatatuliwa kwa sababu upande wa Kupro ya Ugiriki umekataa kutambua haki za Waturuki wa Kupro na umekuwa ukipinga kugawana uwezo wa kisiasa na uchumi na wao.
Wito wa Erdogan wa kutambuliwa
Rais Recep Tayyip Erdogan ametoa wito kwa jamii ya kimataifa kutambua TRNC mara moja katika hotuba yake kwa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa tangu mwaka 2022.
Kufuatia dhifa ya chajio ya pande tatu jijini New York Oktoba 15, 2024, kati ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na viongozi hao wawili wa kisiwa hicho, Umoja wa Mataifa umesema kuwa hakukuwa na muafaka kati ya pande hizo kuhusu suluhu ya suala la Kupro katika mazingira ya sasa.
Wazo la Guterres, ni kuwa mchakato ulianzishwa mwaka 2025 kutambua maeneo ya ushirikiano ambayo yanaweza kufaidi jamii zote mbili katika kisiwa hicho na kujenga imani kwa kuimarisha utamaduni wa ushirikiano.
Mkutano wa kwanza usio rasmi, uliratibiwa na Guterres na kuhudhuriwa na viongozi hao wawili, pamoja na mawaziri wa mambo ya nje wa Uturuki na Ugiriki, ulifanyika jijini Geneva tarehe 17-18, Machi 2025. Washiriki walitambua maeneo sita ya ushirikiano yaliyohitaji kuimarishwa.
Mkutano wa pili wa uratibu kama huo ulifanyika jijini New York tarehe 16-17, Julai 2025, kutathmini hatua zilizopigwa katika maeneo yaliyokubaliwa.
Hata hivyo, hakuna hatua iliopigwa katika masuala muhimu, ikiwemo kufunguliwa kwa vivuko vipya.
Mpango mwingine
Guterres alitembelea kisiwa hicho kwa mara ya kwanza tarehe 27-29 Julai, akifanya mikutano tofauti na viongozi hao wawili.
Katika taarifa kufuatia mikutano hiyo, alisema juhudi katika maeneo ya ushirikiano yaliyokubaliwa zinahitaji kuimarishwa na kutangaza kuwa mkutano mwingine wa mfumo wa 5+1 utaandaliwa baada ya maandalizi thabiti.
Hata hivyo, aliongeza, kuwa hana haja ya mkutano ambao hautakuwa na tija.
Hivi karibuni, Guterres alikuwa na mikutano tofauti na viongozi hao wawili pembeni mwa Mkutano Mkuu wa 81 wa Umoja wa Mataifa.
Hata hivyo, mjumbe binafsi wa Guterres kuhusu Kupro, Maria Angela Holguin Cuellar, anatembelea kisiwa hicho kuanzia Oktoba 29 hadi Novemba 10.
Kama sehemu ya ziara yake, Holguin alikutana tofauti na kiongozi wa Kupro inayosimamiwa na Ugiriki Nikos Christodoulides tarehe 30 Oktoba na Rais wa TRNC Erhurman tarehe 2 Novemba.






















