China imetangaza siku ya Jumatatu kuwa wajumbe wake maalum watatembelea Afrika Kaskazini, Pembe ya Afrika, na Mashariki ya Kati kwa lengo la kuhimiza mazungumzo ya amani na kutuliza uhasama huku migogoro ikiendelea katika kanda mbalimbali.
Wajumbe hao maalum wana lengo la “kuwasilisha mapendekezo” ya Rais wa China Xi Jinping kwa ushirikiano wa wadau wengine katika kutafuta suluhu kwa masuala yanayotatiza Afrika, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje Mao Ning aliwaambia waandishi wa habari jijini Beijing, ikiwemo kuhimiza amani na usalama Mashariki ya Kati.
Mjumbe wa serikali ya China kuhusu Masuala ya Afrika, Liu Xianfa, atatembelea nchini Ethiopia, Djibouti, na Misri kati ya mapema na katikati ya mwezi Novemba, na Hu Changchun, mjumbe maalum wa Masuala ya Pembe ya Afrika, atatembelea nchini Eritrea mapema mwezi Novemba, Mao alisema.
Alisema Zhai Jun, mjumbe wa serikali ya China katika Masuala ya Mashariki ya Kati, atatembelea nchini Iran, Oman, na Saudi Arabia kati ya mapema na katikati mwa mwezi Novemba.
“Diplomasia hii ya wajumbe maalum wa China inalenga kuhimiza mazungumzo ya amani, kutuliza uhasama, na kuwa na nafasi kubwa ya kuimarisha amani na usalama katika kanda,” aliongeza.






















