| Swahili
UTURUKI
3 dk kusoma
Emine Erdogan azindua Jumba la Makumbusho la 'Zero Waste' katika ukumbi wa COP31 nchini Uturuki
Jumba hilo linaonesha safari ya miaka tisa ya Mpango wa Uturuki wa Kutokomeza Taka 'Zero Waste', likiwa na maonesho shirikishi yanayohusu uchakataji wa taka, utunzaji wa rasilimali na uchumi unaozingatia matumizi endelevu ya raslimali.
Emine Erdogan azindua Jumba la Makumbusho la 'Zero Waste' katika ukumbi wa COP31 nchini Uturuki
Emine Erdogan alifungua jumba hilo la makumbusho kwa kukata utepe uliotengenezwa kwa vipande vya vitambaa vilivyokiwisha kutumika. / / Others

Emine Erdogan, mke wa Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Umoja wa Mataifa ya Ngazi ya Juu kuhusu suala la Kutokomeza Taka ‘Zero Waste;, amezindua Jumba la Makumbusho la Zero Waste katika eneo linalofanyika mkutano wa COP31 mjini Antalya. Hafla hiyo iliwakutanisha wake wa viongozi mbalimbali wa dunia pamoja na wageni mashuhuri.

Katika uzinduzi huo uliofanyika Alhamisi, Emine Erdogan alikata utepe wa ufunguzi uliotengenezwa kwa mabaki ya vipande vya vitambaa na kamba za mapambo, kisha kutembelea jumba hilo akiwa ameandamana na viongozi na wageni waliohudhuria.

Wakati wa ziara hiyo, wageni walipata fursa ya kutazama maonesho yanayoelezea historia na maendeleo ya mbinu za kupunguza taka, athari za taka kwa mazingira, hatua za uchakataji, uhifadhi wa rasilimali za asili na umuhimu wa kutumia tena vifaa badala ya kuvitupa.

Samed Ağırbaş, Mkuu wa Taasisi ya Zero Waste na Balozi wa Masuala ya Tabianchi wa COP31, alimfahamisha Emine Erdogan na wageni kuhusu juhudi zinazofanyika kuzuia uzalishaji wa taka pamoja na kutumia tena vifaa ambavyo tayari vimetupwa.

Ziara hiyo ilihitimishwa kwa picha ya pamoja mbeleya mti wa kidijitali, iliyobuniwa kuonesha umuhimu wa kulinda mazingira na kuhifadhi uasilia.

Wawakilishi wa mashirika ya kiraia yanayojihusisha na utunzaji wa mazingira pamoja na vijana pia walionesha mwitikio mkubwa na kuvutiwa na hafla hiyo ya uzinduzi.

Miongoni mwa waliohudhuria walikuwa wake wa marais wa Mauritania, Palau na Maldives, pamoja na wake wa mawaziri wakuu wa Burundi, Eswatini na Visiwa vya Solomon.

Wengine waliohudhuria ni Amina El-Dilawi, mke wa Waziri Mkuu wa Libya, akiwa pamoja na binti yake Estabrak Abdulhamid Al Dbeibah; Tunku Azizah Aminah Maimunah Iskandariah, mke wa Sultan wa jimbo la Pahang nchini Malaysia; pamoja na Leyla Aliyeva, binti wa Rais wa Azerbaijan, aliyeambatana na Alyona Aliyeva.

Aidha, wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Umoja wa Mataifa ya Ngazi ya Juu kuhusu Zero Waste walishiriki katika hafla hiyo. Viongozi wengine waliohudhuria ni Waziri wa Familia na Huduma za Kijamii wa Uturuki, Mahinur Özdemir Göktaş; Waziri wa Mazingira, Miji na Mabadiliko ya Tabianchi, Murat Kurum; pamoja na Meya wa Gaziantep, Fatma Şahin.

Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na watu mashuhuri kutoka katika sekta za sanaa, burudani na michezo.

Maonesho ya safari ya Uturuki katika utekelezaji wa ‘Zero Waste’

Jumba hilo limeanzishwa kwa lengo la kuitambulisha jumuiya ya kimataifa maarifa, uzoefu na mbinu mbalimbali ambazo Uturuki imekusanya katika kipindi cha utekelezaji wa Mpango wake wa ‘Zero Waste’.

Maonesho yaliyomo ndani yake yanaelezea safari ya miaka tisa ya mpango huo, mafanikio yaliyopatikana ndani na nje ya nchi, pamoja na mipango inayolenga kuimarisha dhana ya uchumi unaozingatia matumizi endelevu ya raslimali, ambapo rasilimali hutumika tena badala ya kutupwa.

Jengo hilo limebuniwa kwa kuzingatia dhana ya usanifu wa majani matano. Ndani yake kuna maeneo ya maonesho shirikishi, matumizi ya teknolojia za kidijitali na kazi mbalimbali za sanaa zinazofafanua masuala ya usimamizi wa taka, uchakataji, uhifadhi wa rasilimali na matumizi mapya ya vifaa vilivyokwisha tumika.

Wageni wanaotembelea jumba hilo pia wana nafasi ya kurekodi ujumbe wa video kwa ajili ya vizazi vijavyo kupitia eneo maalumu linaloitwa “2035 Message Wall” (Ukuta wa Kutuma Ujumbe wa 2035).

Sehemu nyingine ya kipekee ni “Commitment Tree” (Mti wa Ahadi), uliojengwa kuzunguka mzeituni wenye umri wa zaidi ya miaka 30.

Kupitia sehemu hiyo, wageni wanaalikwa kuandika ahadi zao za kulinda mazingira kwa mwaka 2035 kwenye karatasi zenye umbo la majani, kisha kuzibandika kwenye mti huo.

Zoezi hilo linalenga kuwakutanisha watu katika kutoa mchango wa pamoja kuelekea kujenga mustakabali endelevu na unaozingatia uhifadhi wa mazingira.

CHANZO:AA