Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, amezitaka nchi zilizoendelea kuchukua wajibu mkubwa zaidi katika kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi na kutoa ufadhili wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Amesisitiza kuwa ufadhili huo unapaswa kupatikana kwa urahisi zaidi, kuwa wa uhakika na kuzingatia mahitaji ya nchi husika.
Erdogan alitoa kauli hiyo Jumatano, wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Viongozi wa COP31 uliofanyika mjini Antalya, katika jimbo la kusini mwa Uturuki.
"Nchi zilizoendelea ambazo kihistoria zimetumia sehemu kubwa ya kiwango cha hewa ukaa kinachoweza kuzalishwa duniani zinapaswa kuchukua jukumu kubwa zaidi katika kupunguza uzalishaji wa gesi hizo na kutoa ufadhili," alisema Erdogan.
Ameonya kuwa dunia inakabiliwa na changamoto zinazozidi kuongezeka, zikiwemo ongezeko la joto duniani, kupotea kwa bioanuwai, matumizi ya kupita kiasi ya rasilimali za asili, vitisho kwa usalama wa chakula na majanga yanayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi ambayo yanazidi kuwa makubwa na yenye uharibifu.
Erdogan ametoa wito wa kuboreshwa kwa upatikanaji wa fedha, teknolojia na fursa za kujengewa uwezo, hususan kwa nchi zenye maendeleo duni na mataifa madogo ya visiwani yanayoendelea.
"Tumeainisha suala la kufanya mahitaji ya nchi za Pasifiki yaonekane zaidi na kuyaweka katika nafasi ya kipaumbele kuwa jukumu letu la msingi," alisema.
Akieleza kuhusu dhamira ya Uturuki katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, Erdogan amesema nchi hiyo inaendelea kutekeleza mikakati ya kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi katika sekta mbalimbali, kuanzia nishati na viwanda hadi usafirishaji na kilimo, huku mabadiliko kuelekea uchumi wa kijani yakiwa kipaumbele katika uchumi wake wote.
"Ustaarabu wetu umejengwa juu ya msingi wa kuheshimu mazingira, na Dunia ni amana takatifu ambayo lazima ilindwe na kuhifadhiwa," aliongeza.
Kuondoa gesi chafuzi
Erdogan alisisitiza tena dhamira ya Uturuki ya kuondoa gesi chafuzi ifikapo mwaka 2053, akisema masuala ya mazingira yanaingizwa katika mipango ya maendeleo na sera za usalama wa nishati.
Akizungumzia mpango wa Kutokuwepo Taka, ulioanzishwa mwaka 2017, Erdogan alisema kiwango cha urejelezaji wa taka nchini Uturuki kimeongezeka kutoka takribani asilimia 13 hadi karibu asilimia 40 mwishoni mwa mwaka 2025.
Amesema nchi hiyo inalenga kupata tija katika maeneo 10 ya waliyoyapa kipaumbele, yakiwemo kuelekea nishati safi, udhibiti wa taka, usalama wa chakula, maendeleo ya viwanda, ujenzi wa miji inayoweza kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na ulinzi wa bahari.
Ameongeza kuwa katika kipindi cha miaka 10 ijayo, Uturuki inalenga kuongeza kiwango cha matumizi ya umeme kwa asilimia 50, kupunguza kwa nusu kasi ya ongezeko la uzalishaji wa taka na kupanua matumizi ya malighafi zinazoweza kutumika tena katika sekta ya viwanda.
Gaza: Uhalifu wa kuangamiza mazingira
Akizungumzia hali ya Gaza, Erdogan alilaani mashambulizi ya Israel, akisema yamesababisha uharibifu mkubwa wa mazingira pamoja na kusababisha vifo vya watu watu wengi.
"Kama nilivyosisitiza katika hotuba yangu mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, yaliyotokea Gaza si mauaji ya halaiki pekee, bali pia ni uhalifu wa kuangamiza mazingira," alisema.
Ametaja uharibifu wa miti ya mizeituni iliyokuwa hapo karne nyingi, uchafuzi wa udongo na maji, pamoja na miji mizima kugeuzwa vifusi.
Erdogan pia alieleza kuongezeka kwa janga la kibinadamu katika eneo hilo kufuatia mvua kubwa na mafuriko, akisema makumi ya maelfu ya mahema na makazi ya muda yalikuwa yamezama ndani ya maji kutokana na mafuriko hayo, huku miundombinu mingi ikiwa imeharibiwa.
"Mamia ya maelfu ya ndugu na dada zetu huko Gaza, ambao hawana makazi, hususan watoto wasio na hatia wanaotetemeka kwa baridi, wanahangaika kuendelea kuishi ndani ya maji katika mazingira ya majira baridi, mara nyingi wakiwa hawana wazazi wao," alisema.
Erdogan alisisitiza kuwa wote waliyeshuhudia au kufahamu hali hiyo hawawezi kukwepa kuwajibishwa.
Alitoa wito wa kuwasilishwa mara moja kwa misaada ya kibinadamu huko Gaza, kukomeshwa kwa hali ya kulitenga eneo hilo na kusitishwa kwa mateso yanayowakabili Wapalestina.
"Kuonyesha nguvu kupitia mateso ya watoto wa Gaza, kwa kweli, ni ishara ya udhaifu, kutokuwa na uwezo na, zaidi ya yote, ukosefu wa dhamiri," alisema Erdogan.
Akihitimisha hotuba yake, alisisitiza kuwa ni muhimu kuyaachia vizazi vijavyo dunia safi zaidi, yenye mazingira bora na haki zaidi, kabla sayari hii haijafikia hatua ya kutofaa tena kwa maisha ya binadamu.























