| Swahili
UTURUKI
5 dk kusoma
COP31 ANTALYA: African Culture House na OAFLAD zasaini hati ya makubaliano
Hati hiyo ya makubaliano ni hatua muhimu katika kuunganisha juhudi za African Culture House za kufikia jamii moja kwa moja na kuwawezesha wanawake na mtandao wa ushirikiano wa OAFLAD unaohusisha bara zima la Afrika.
COP31 ANTALYA: African Culture House na OAFLAD zasaini hati ya makubaliano
Hafla ya utiaji saini ilifanyika katika Jumba la Makumbusho la Kutokomeza Taka (Zero Waste), lililopo ndani ya eneo la mkutano. / / TRT Swahili

Shirika la Wake wa Marais wa Afrika linalojihusisha na Maendeleo (OAFLAD) na African Culture House zimesaini hati ya makubaliano (MoU) yenye lengo la kuwezesha uwezo wa wanawake kiuchumi na nafasi yao katika kijamii.

Hati hiyo imesainiwa pembezoni mwa Mkutano wa 31 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Mfumo wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC), unaoendelea kufanyika Antalya, nchini Uturuki.

Hafla ya utiaji saini ilifanyika katika Jumba la Makumbusho la Kutokomeza Taka (Zero Waste), lililopo ndani ya eneo la mkutano. Waliohudhuria ni pamoja na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Balozi Musa Kulaklıkaya; Balozi Yönet Can Tezel, Mkurugenzi Mkuu anayeshughulikia Afrika ya Kusini na Masuala ya Kimataifa; Zeliha Sağlam, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya African Culture House; pamoja na Dkt. Nardos Berhanu Wudeneh, Katibu Mtendaji wa OAFLAD.

Hati hiyo ya makubaliano ni hatua muhimu katika kuunganisha juhudi za Africa Culture House za kufikia jamii moja kwa moja na mtandao wa ushirikiano wa OAFLAD unaoenea katika bara zima la Afrika. Hati hiyo ilisainiwa na Zeliha Sağlam na Dkt. Nardos Berhanu Wudeneh.

Akizungumza katika hafla hiyo, Zeliha alimshukuru Emine Erdogan, mke wa Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na ambaye pia ni Rais wa Heshima wa African Culture House, kwa dhamira yake thabiti ya kupanua wigo wa shughuli na mchango wa chama hicho nje ya Uturuki na katika nchi za Afrika. Pia alimshukuru Fatima Maada Bio, mke wa Rais wa Sierra Leone Julius Maada Bio na Rais wa Heshima wa OAFLAD, kwa kuendelea kutoa msaada wake.

“Makubaliano haya tunayotarajia kusaini leo yanaashiria dhamira yetu ya kujenga dunia yenye ustawi na haki kwa wanawake nchini Uturuki na katika nchi za Afrika,” alisema Zeliha.

Amesema kuwa African Culture House ilianzishwa mwaka 2016 kama mpango wa uwajibikaji kwa jamii, chini ya uongozi wa Emine Erdogan, Zeliha alieleza kuwa Mke wa Rais wa Uturuki alivutiwa sana na kujituma pamoja na juhudi za wanawake wa Afrika alipokuwa akiandamana na Rais Recep Tayyip Erdogan katika ziara zake katika nchi za Afrika.

Baada ya ziara hizo, Emine Erdogan aliamua kuanzisha jukwaa nchini Uturuki kwa ajili ya kutambua na kuthamini mchango pamoja na matarajio ya wanawake wa Afrika, huku likitoa nafasi ya kuonesha uzoefu na ujuzi wao.

Zeliha alibainisha kuwa kituo hicho kimekuwa kikitanua shughuli zake hatua kwa hatua, na sasa zinajumuisha mijadala ya kitaaluma, warsha za utamaduni na maonesho ya kisanii.

“Tangu wakati huo, tumepiga hatua nyingi muhimu, na leo tunakaribia kufikia hatua nyingine kubwa kwa kushirikiana na mshirika wetu, OAFLAD,” alisema.

“Tunapata hamasa kutokana na uongozi wa kimataifa wa Emine Erdogan”

Katibu Mtendaji wa OAFLAD, Dkt. Nardos Berhanu Wudeneh, alieleza furaha yake ya kushiriki katika hafla hiyo kwa niaba ya shirika hilo.

“Napenda kutoa shukrani zetu za dhati kwa African Culture House kwa kutuunganisha pamoja na kwa ukarimu mkubwa tuliopokelewa nao tangu tulipowasili Antalya,” alisema.

Wudeneh alipongeza kurasimishwa kwa ushirikiano huo, akieleza kuwa utasaidia kuimarisha juhudi za pamoja katika kuwawezesha wanawake kiuchumi, kuhifadhi kazi za mikono za jadi na kuandaa fursa kwa wanawake wazalishaji pamoja na vyama vya ushirika katika maeneo mbalimbali ya Afrika.

“Makubaliano haya yanasainiwa katika kipindi muhimu sana, wakati wa mkutano wa COP31, ambapo dunia inaendelea kutoa kipaumbele zaidi kwa athari za mabadiliko ya tabianchi, na kuhusu suala la haki katika maisha na ustawi wa wanawake na wasichana,” alisema.

Akisisitiza kuwa taasisi zote mbili zinatambua umuhimu wa kuwashirikisha wanawake kama kiini cha suluhisho la changamoto za tabianchi, Wudeneh aliongeza: “Tunapata hamasa kutokana na uongozi wa kimataifa wa Mke wa Rais Emine Erdogan, ambaye mpango wake wa Kutokomeza Taka (Zero Waste), hususan, umekuwa mfano madhubuti wa maendeleo endelevu.”

Bidhaa zinazotengenezwa na wanawake wa Afrika kuuzwa kwa haki na usawa

Akizungumza baada ya hafla ya utiaji saini, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Balozi Musa Kulaklıkaya, alisisitiza kuwa mkutano huo ni matokeo ya mawasiliano na juhudi za miezi kadhaa zilizofanywa na pande zote husika.

Alitoa shukrani zake kwa Emine Erdogan kwa dhamira yake thabiti ya kupanua wigo wa shughuli za African Culture House nje ya Uturuki na katika nchi za Afrika, pamoja na msaada wake endelevu.

Kulaklıkaya alieleza kuwa African Culture House iliyopo Ankara inawakilisha hatua ya awali katika kuanzisha njia za kubadilishana utamaduni kati ya Uturuki na nchi za Afrika, hususan kupitia juhudi za wanawake.

Alifafanua kuwa bidhaa zinazotengenezwa na wanawake katika nchi mbalimbali za Afrika hununuliwa na kuuzwa kwa wanunuzi kwa usawa na haki.

Akibainisha kuwa kwa sasa African Culture House ina bidhaa zilizotengenezwa na mikono kutoka zaidi ya nchi 40 za Afrika, Kulaklıkaya alisema kuwa mapato yanayotokana na mauzo hayo hutumika kusaidia miradi inayowanufaisha wanawake na watoto katika maeneo mbalimbali ya Afrika.

Kulaklıkaya alielezea makubaliano yaliyofikiwa na OAFLAD kuwa mafanikio mengine makubwa, akisema: “Kupitia makubaliano haya, pande zote mbili zinalenga kufungua masoko ya haki kwa wanawake wazalishaji, kuhakikisha kazi zao zinatambuliwa na kuthaminiwa ipasavyo, kuandaa miradi mipya inayokidhi mahitaji ya maendeleo ya maeneo mbalimbali, na kuwasaidia wanawake kubuni mipango inayozingatia vipaumbele vyao wenyewe.

“Huu si ushirikiano tu kati ya taasisi mbili; ni daraja linalounganisha juhudi na bidii ya wanawake na fursa ambazo kwa muda mrefu wamekuwa wakistahili kuzipata.”