Tume ya Umoja wa Afrika imetoa wito kwa Ethiopia, Eritrea na Misri kuwa watulivu na kujiepusha na uhasama au taarifa ambazo zinaweza kutatiza amani katika kanda na uthabiti.
"Tume inaomba nchi zote tatu kushughulikia tofauti zao kupitia njia za kidiplomasia na majadiliano ya amani," ilisema katika taarifa siku ya Alhamisi.
Siku ya Alhamisi, Ethiopia iliagiza kufungwa kwa ubalozi wake nchini Eritrea na kuwatimua maafisa 10 wa ubalozi wa Eritrea, kufanya Eritrea kusitisha uhusiano wa kidiplomasia na jirani zake.
Pia ilimtaka mwanadiplomasia mmoja wa Misri kuondoka nchini humo katika muda wa saa 48, na Misri ikamtimua afisa wa ubalozi wa Ethiopia nchini mwao na kumpa saa 48 kuondoka pia.
Majibizano
Eritrea ilisema kuwa inasitisha uhusiano wa kidiplomaisa na jirani zake Ethiopia siku ya Alhamisi, kutokana na maafisa wao kutimuliwa kutoka Ethiopia.
"Eritrea haina budi ila kujibu yaliyojiri na kusitisha uhusiano na Ethiopia na matokeo yote hasi yanayohusiana na hali hiyo," wizara yake ya mambo ya nje ilisema katika taarifa kwenye mtandao wa X.
Wakati huohuo, Misri imekanusha kuingilia masuala ya ndani ya nchi yoyote, kufuatia madai ya Ethiopia ya kuunga mkono makundi yenye silaha kaskazini mwa nchi.
















