Mhandisi wa umeme wa Wizara ya Nishati ya Marekani amekamatwa kwa tuhuma za kutoa msaada kwa kundi la Wa-Houthi nchini Yemen kwa kununua vifaa vinavyodaiwa kutumika kutengeneza vilipuzi na ndege zisizo na rubani, pamoja na kusafiri kwenda Yemen, vyombo vya habari vya Marekani viliripoti Ijumaa.
Kwa mujibu wa shirika la habari la CBS News, likinukuu Wizara ya Sheria ya Marekani, Ellaboudy alikamatwa Alhamisi na anatarajiwa kufikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Ijumaa.
Ellaboudy alijaribu kuwasaidia Wa-Houthi kuimarisha uwezo wao wa mawasiliano na kusafiri hadi Yemen mwezi Septemba mwaka jana, CBS News ilinukuu Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI).
“Ellaboudy alitumia pasipoti aliyopewa alipokuwa akifanya kazi katika Kikosi cha Wahandisi cha Jeshi la Marekani ili kusafiri hadi Oman, nchi inayopakana na Yemen ,” CBS News ilinukuu Wizara ya Sheria ikisema.
Ellaboudy anakabiliwa na mashitaka chini ya sheria ya Marekani inayoharamisha kutoa msaada wa vifaa au rasilimali kwa makundi yaliyotajwa na serikali ya Marekani kuwa makundi ya kigaidi. Na kundi la Wa-Houthi ni miongoni mwa makundi yaliyoorodheshwa kuwa magaidi.
Iwapo atapatikana na hatia, Ellaboudy anaweza kuhukumiwa kifungo cha hadi miaka 20 jela, kwa mujibu wa Wizara ya Sheria ya Marekani.
Yemen imekuwa katika mzozo wa muda mrefu tangu Wa-Houthi walipouteka mji mkuu, Sanaa, pamoja na majimbo kadhaa mwaka 2014.
Hatua hiyo ilisababisha muungano ulioongozwa na Saudi Arabia kuingilia kati mwaka 2015, ukiunga mkono serikali ya Yemen inayotambuliwa kimataifa.




















