| Swahili
AFRIKA
1 dk kusoma
Maporomoko katika jalala yasababisha vifo vya watu wasiopungua 30 Guinea
Shughuli za uokoaji zinaendelea baada ya sehemu ya jalala kuporomoka na kuharibu nyumba katika mji mkuu wa Guinea kufuatia mvua kubwa.
Maporomoko katika jalala yasababisha vifo vya watu wasiopungua 30 Guinea
Wakazi na waokoaji wakitafuta miili kwenye jalala eneo la Dar es Salaam mjini Conakry, Agosti 2026. / AFP / AFP

Watu wasiopungua thelathini walifariki katika ajali ya kuporomoka kwa jalala katika mji mkuu wa Guinea siku ya Jumapili kufuatia mvua kubwa ilionyesha, serikali ilisema.

Wengine sita walijeruhiwa katika ajali hiyo wilaya ya Bbessia, eneo la Dar-es-salam, viungani mwa mji mkuu, taarifa ya serikali ilisema.

"Tumewapeleka maafisa wetu kwa ajili ya shughuli za uokoaji kutafuta watu ambao wanaweza kuwa wamefukiwa, na pia kuondoa miili," serikali iliongeza.

Waziri Mkuu Amadou Oury Bah alitembelea eneo hilo la ajali, ambapo shughuli za uokoaji zilikuwa zinaendelea.

Hatua zimechukuliwa "kuhakikisha kuwa waliojeruhiwa wanatibiwa" na "kutoa msaada kwa walioathirika na mkasa huo", serikali ilisema katika taarifa.

Kabla idadi rasmi ya waliofariki kutolewa, kiongozi wa eneo hilo Lancine Sylla alisema kuwa anahofia watu wengi zaidi huenda walifariki.

"Tumetoa miili 18 ambayo imepelekwa kwenye chumba cha kuhifadhi maiti," alisema.

Mmoja wa kiongozi wa upinzani wa Guinea, aliyekuwa waziri mkuu Cellou Dalein Diallo, ambaye anaishi uhamishoni, ameitaja ajali hiyo kuwa "mkasa wa kustua zaidi".

CHANZO:TRT Afrika Swahili