Iran itakubali tu “makubaliano ya haki na ya kina” katika mazungumzo yake na Marekani kuhusu kumaliza vita vya Mashariki ya Kati, waziri wa mambo ya nje wa Iran amesema.
“Tutafanya kila tuwezalo kulinda haki na maslahi yetu halali katika mazungumzo,” Waziri wa Mambo ya Nje Abbas Araghchi alisema mjini Beijing baada ya kukutana na mwanadiplomasia mkuu wa China Wang Yi, vyombo vya habari vya Iran vimeripoti.
“Tunakubali tu makubaliano ya haki na yanayojumuisha masuala yote.”
Rais wa Marekani Donald Trump hapo awali alisema alikuwa anasimamisha mpango wa kijeshi wa Marekani wa kusindikiza meli kupitia Mlango wa Hormuz baada ya siku moja tu ya kutangaza kuanza kwa operesheni hio, katika juhudi za kufikia makubaliano na Iran kumaliza vita vya Mashariki ya Kati.
Akiashiria kupokea maombi kutoka Pakistan na nchi nyingine, pamoja na hatua iliyopigwa kuelekea makubaliano ya mwisho na Iran, Trump alitangaza uamuzi huo mpya lakini akasisitiza kuwa zuio la majini litaendelea kikamilifu.
“Tumeafikiana kwa pamoja kwamba, ingawa zuio litaendelea kutumika kikamilifu, Operesheni ya ‘Project Freedom’ itasitishwa kwa muda mfupi ili kuona kama makubaliano yanaweza kukamilishwa na kusainiwa,” Trump aliandika kwenye mitandao ya kijamii.
Araghchi hakujibu moja kwa moja pendekezo la Trump kama motisha ya kusaidia kufikia makubaliano kati ya pande hizo mbili.
Safari ya Araghchi inakuja kabla ya ziara iliyopangwa ya Rais wa Marekani Donald Trump nchini China tarehe 14–15 Mei kukutana na Rais Xi Jinping, safari ambayo aliiahirisha baada ya Marekani na Israel kushambulia Iran.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio Jumanne alitoa wito kwa China kumshinikiza Araghchi kulegeza msimamo wa Iran kuhusu Mlango wa Hormuz, ambao unatumiwa kupitisha takriban theluthi moja ya mafuta duniani.
“Natumai Wachina watamwambia (Araghchi) kile anachopaswa kuambiwa, nacho ni kwamba kile mnachofanya kwenye mlango huo kinawafanya mtengwe kimataifa,” Rubio aliwaambia waandishi wa habari.
Wang Yi badala yake alielezea mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran kama “yasiyo halali” wakati wa mkutano wake na mwenzake wa Iran, kulingana na shirika la habari la Iran Tasnim News Agency.
Waziri huyo wa mambo ya nje wa China pia alimwambia mwenzake wa Iran kwamba China “imehuzunishwa sana” na vita hivyo vilivyodumu zaidi ya miezi miwili na akasema kwamba kuna haja ya kusitishwa kamili kwa mapigano.
“Tunaamini kwamba kusitishwa kamilia kwa mapigano kunahitajika kwa haraka, na kwamba kurejea kwa mapigano hakukubaliki, ni muhimu sana kuendelea kujikita kwenye mazungumzo na majadiliano,” Wang alisema, kwa mujibu wa video ya mkutano huo.
















