Ni nini hutokea wakati Bahari ya Pasifiki inapopata joto lisilo la kawaida?
Huenda ikaonekana kama ni jambo linalotokea maelfu ya kilomita mbali na Afrika.
Lakini ongezeko hili la joto linaweza kuwa na athari za mifumo ya hali ya hewa duniani kote — ikiwemo barani Afrika.
Tunazungumzia El Niño.
Na nchi kadhaa barani tayari zinajiandaa kwa athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua kubwa zinazotabiriwa.
Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) linasema kuwa El Niño inayotarajiwa katika miezi ijayo inaweza kuwa na nguvu zaidi kuwahi kurekodiwa katika miongo minne iliyopita.
"Utabiri huu unaonesha uwezekano mkubwa sana wa karibu asilimia 100 kwamba El Niño itaendelea hadi Februari 2027," Celeste Saulo, Katibu Mkuu, Shirika la Hali ya Hewa Duniani alisema wakati shirika hilo la WMO lilikuwa linatoa tahadhari ya El nino.
Athari tofauti za El Nino
Lakini El Nino haiathiri kila nchi kwa namna moja.
Athari zake hutegemea eneo, msimu na nguvu ya tukio husika la El Niño.
Katika Kusini mwa Afrika, El Niño mara nyingi uhusishwa na mvua pungufu ya kiwango cha kawaida wakati wa msimu mkuu wa mvua.
Hali hii inaweza kusababisha ukame, uhaba wa maji, kupungua kwa uzalishaji wa mazao, kupotea kwa mifugo na kuongezeka kwa uhaba wa chakula.
Lakini katika eneo la Afrika Mashariki, hali inaweza kuwa tofauti kabisa.
Matukio fulani ya El Nino huleta mvua nyingi kupita kiasi, na kuongeza hatari ya mafuriko na maporomoko ya ardhi.
Nchi zikiwemo Kenya, Tanzania, Uganda, Rwanda, Burundi, Somalia na maeneo ya Ethiopia zinaweza kukumbwa na mabadiliko makubwa ya mvua wakati wa matukio ya El Niño, jambo linalosababisha majanga yenye madhara makubwa.
Hofu hiyo imepelekea baadhi ya viongozi kutoa tahadhari ikiwemo Tanzania.
"Kuna mambo ambayo tunafaa kuyachukulia hatua kwa haraka tusisubiri; tukisubiri, sisi wenyewe tutashindwa kufika huko, "Deogratius John Ndejembi, Makamu wa Rais, Tanzania aliambia mashiria tofauti ya serikali mwezi Oktoba.
Wakati kipindi cha El Niño kikikaribia, nchi zinaimarisha hatua za kujiandaa.
Nchini Kenya, serikali imepewa na Benki Kuu ya Dunia kiasi cha takriban Dola za Marekani milioni 400 kama fedha za dharura kwa ajili ya kusaidia kukabiliana na athari za El Nino.
Tayari nchini Kenya, Serikali imezitambua kaunti 18 kama maeneo yatakayokuwa katika hatari kubwa, zikiwemo kaunti za ukanda wa pwani kama vile Mombasa.
Mjini Mombasa, mamlaka zimeanza kuandaa vituo vya uokoaji wa dharura na kuimarisha uratibu na mashirika muhimu.
"Ukumbi wetu wa kijamii utageuzwa kuwa vituo vya hifadhi na uokoaji. Iwapo lolote litatokea, tumeshirikiana na Jeshi la Wanamaji, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege ya Kenya pamoja na Mamlaka ya Bandari ya Kenya ili kuhakikisha kuwa huduma kama vile magari ya wagonjwa na vifaa vya kuzima moto viko tayari,” Abdulswamad Nassir, Gavana wa Kaunti ya Mombasa aliwaambia waandishi wa habari Oktoba.
Kaunti hiyo pia imetoa amri ya kusitisha shughuli za ujenzi ikiwemo marufuku ya kuchanganya mchanga na kokoto katika maeneo ya ujenzi kama hatua ya kuzuia mafuriko.
"Uidhinishaji wa sasa wa majengo unaonesha kuwa yeyote anayetaka kujenga anapaswa kutumia zege iliyochanganywa tayari (pre-mixed concrete). Hii ina maana kwamba kuchanganya zege, kokoto na saruji eneo la ujenzi hakukubaliki tena,” Gavana aliongezea.
Mikakati tofauti katika nchi za Afrika Mashariki
Kenya pia imezindua mpango wa Shilingi bilioni 2.1 kulinda wafugaji katika kaunti 24 dhidi ya hasara zitakazojitokeza, milipuko ya magonjwa na mafuriko yanayohusiana na El Nino.
Nchi nyingi zinataka kutumia uzoefu wa uharibifu ulioshuhudiwa wakati wa El Nino ya mwaka 2023 na mafuriko yaliyosababishwa mwaka 2024 kuepuka kujirudia kwa hasara ya maisha ya binadamu na mifugo.
Katika nchi jirani ya Tanzania, serikali imetenga Shilingi bilioni 730 kwa ajili ya maandalizi ya kukabiliana na majanga, hatua za dharura na ukarabati wa miundombinu muhimu.
Mamlaka pia zinazihimiza jamii kuandaa mifumo ya mifereji ya maji taka na kusafisha njia za maji taka kabla ya mvua kubwa kuanza kunesha.
"Ninataka mfanye kampeni ya haraka kuhakikisha mikondo yetu ya maji, mitaro yetu inafanyiwa... maeneo yoyote ambayo yamesafishwa drainage, ule uchafu ulioondolewa kule uende uondolewe, kabla mvua haijawa kubwa, hizo za El Niño tunazotarajia, " aliagiza Ndejembi, Makamu wa Rais waTanzania.
Serikali pia inaangazia madaraja, makaravati na miundombinu mingine ambayo inaweza kuzidiwa na mvua kubwa.
Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania inaimarisha hatua za dharura katika viwanja vya ndege, mifumo ya umeme mbadala na njia za mawasiliano ili kupunguza hatari ya usumbufu mkubwa.
Maghala ya vifaa vya tiba pia yameelekezwa kuhifadhi dawa muhimu ili kujiandaa kwa ongezeko la mahitaji ya dharura.
Nchini Somalia, Shirika la Kudhibiti Majanga limetambua miji 29 katika mikoa 14 iliyo katika hatari ya kukumbwa na mvua kubwa zinazoweza kusababisha mafuriko kutokana na hali inayotarajiwa ya El Niño.
Serikali inawahimiza wananchi wake kuhama maeneo ya karibu na mito kama vile Shebelle, ambayo hujulikana kwa kufurika na kuvunja kingo zake wakati wa mvua nyingi kupita kiasi.
Uganda, Rwanda na Burundi pia zimetoa tahadhari, huku mamlaka zikizihimiza jamii kusafisha mifumo ya mifereji ya maji na kuwahimiza watu wanaoishi katika maeneo hatarishi kwa mafuriko kuhamia maeneo salama.
Bara hili lina uzoefu wa moja kwa moja na madhara ya El Nino
Tukio kubwa la hivi karibuni zaidi la El Nino kuikumba Afrika Mashariki lilikuwa la mwaka 2023–2024, ambapo mvua kubwa zilisababisha mafuriko makubwa katika nchi kadhaa, zikiharibu nyumba, barabara na mashamba pamoja na kuvuruga shughuli za kujipatia kipato.
Mafunzo ya misimu ya El Nino ya awali
Hili linatoa funzo muhimu.
Madhara ya awali ya El Niño yameonesha umuhimu wa kuwa na miundombinu bora, timu imara zaidi za kukabiliana na dharura, mipango ya kuhama maeneo hatarishi na mifumo ya tahadhari ya mapema.
Wakulima nao wanahitaji taarifa kwa wakati muafaka kuhusu wakati wa kupanda, aina ya mazao yanayofaa zaidi kwa hali inayotarajiwa, na jinsi ya kukabiliana na mvua nyingi kupita kiasi.
Mafuriko yanaweza pia kuleta mazingira yanayochochea kuenea kwa magonjwa kama vile kipindupindu na malaria.
Mashirika ya kikanda, yakiwemo IGAD na ICPAC, yana jukumu muhimu la kusaidia serikali kubadilishana taarifa za hali ya hewa, utabiri, tahadhari na mipango ya maandalizi.
Ushirikiano huu wa kikanda ni muhimu kwa sababu madhara ya El Nino yanavuka mipaka nchi moja hadi nyengine.
Mfumo mmoja wa hali ya hewa unaweza kuathiri nchi kadhaa kwa wakati mmoja.
Lakini kujiandaa kwa El Nino hakuhusu tu utabiri wa hali ya hewa na timu za dharura.
Pia kunahusu maandalizi ya kifedha.
Kukabiliana na maafa kunahitaji rasilimali kubwa za kifedha, na nchi za Afrika zinatakiwa kubuni njia mbalimbali zitakazohakikisha wa rasilimali kwa wakati.
Kwa jamii nyingi barani Afrika, madhara ya El Nino itakuwa ni kipimo tosha iwapo serikali zitakuwa zimejiandaa vya kutosha kukabiliana na majanga makubwa kwa sasa na baadae.






















