| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
Tanzania: Waziri Mkuu asisitiza ushirikiano wa kikanda kukabiliana na uhalifu wa kimataifa
Kulingana na Nchemba, katika dunia ya sasa, aina nyingi za uhalifu hupangwa, hufadhiliwa na kuratibiwa kwa njia za kidijitali, hali inayohitaji mifumo imara ya kiteknolojia pamoja na ushirikiano wa pamoja ili kuudhibiti kwa ufanisi.
Tanzania: Waziri Mkuu asisitiza ushirikiano wa kikanda kukabiliana na uhalifu wa kimataifa
Waziri Mkuu wa Tanzania, Mwigulu Nchemba./Picha:Wengine / Others

Waziri Mkuu wa Tanzania Mwigulu Nchemba, amesema ushirikiano wa kikanda na kimataifa ni sharti la mafanikio katika mapambano dhidi ya uhalifu wa kimataifa unaozidi kubadilika na kuvuka mipaka.

Kulingana na Nchemba, katika dunia ya sasa, aina nyingi za uhalifu hupangwa, hufadhiliwa na kuratibiwa kwa njia za kidijitali, hali inayohitaji mifumo imara ya kiteknolojia pamoja na ushirikiano wa pamoja ili kuudhibiti kwa ufanisi.

“Kama ambavyo uhalifu uliopangwa hauwezi kuwepo bila kuvuka mipaka, vivyo hivyo vyombo vya dola na mifumo ya haki ya jinai haviwezi kukabiliana nao kwa ufanisi bila kuwa na mifumo madhubuti ya ushirikiano wa kimataifa, hususan katika maeneo ya msaada wa kisheria na urejeshaji wa watuhumiwa,” amesema Waziri Mkuu huyo  wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 11 na Kongamano la Chama cha Waendesha Mashtaka Afrika Mashariki (EAAP), Mei 04, 2026 jijini Dar es Salaam.

Nchemba alisisitiza matumizi ya teknolojia kama sehemu muhimu ya mafanikio katika mapambano hayo, akibainisha kuwa ni vigumu kufanikiwa katika mapambano hayo bila matumizi ya teknolojia.

Akielezea hatua zilizochukuliwa na Tanzania, Nchemba alisema kuwa serikali ya nchi hiyo imeendelea kuboresha mifumo ya kisheria ili kuimarisha ushirikiano wa kimataifa.

“Serikali ya Tanzania imepitia sheria zake za msaada wa kisheria ili kupanua wigo wa ushirikiano, ikiwemo matumizi ya ushahidi wa kidijitali, ufuatiliaji wa mawasiliano na mbinu za kisasa za uchunguzi,” ameeleza.

CHANZO:TRT Afrika Swahili