| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
Umoja wa Mataifa waonya kuhusu hali tete eneo linalozozaniwa kati ya Sudan na Sudan Kusini
Afisa mmoja mwandamizi wa Umoja wa Mataifa ameonya Baraza la Usalama kuwa hali ya usalama katika eneo linalozozaniwa la Abyei kati ya Sudan na Sudan Kusini imekuwa mbaya zaidi katika kipindi cha miezi sita iliopita.
Umoja wa Mataifa waonya kuhusu hali tete eneo linalozozaniwa kati ya Sudan na Sudan Kusini
Serikali zote za Sudan na Sudan Kusini zinadai umiliki wa eneo la Abyei lenye utajiri wa mafuta. / AA

Afisa mmoja mwandamizi wa Umoja wa Mataifa ameonya Baraza la Usalama kuwa hali ya usalama katika eneo linalozozaniwa la Abyei kati ya Sudan na Sudan Kusini imekuwa mbaya zaidi katika kipindi cha miezi sita iliopita.

Martha Ama Akyaa Pobee, Katibu Mkuu Msaidizi wa Afrika katika Idara za Siasa na Masuala ya Amani (DPPA-DPO), amewaambia wajumbe wa Baraza kuwa hali ya kisiasa Abyei bado imeathiriwa na vita vya Sudan na ukosefu wa usalama Sudan Kusini.

"Hakuna hatua zilizopigwa na nchi zote mbili katika kutatua mzozo kuhusu usimamizi wa eneo la Abyei," Pobee alisema.

Pobee aliongeza kuwa hali ya usalama Abyei imekuwa mbaya katika kipindi cha miezi sita iliopita, zaidi kutokana na uhalifu, kuenea kwa silaha haramu na kuwepo kwa watu wenye silaha, "ambavyo vimefanya hali kuwa tete zaidi."

Vifo na majeruhi

Pobee alisema kuwa Kikosi cha Muda cha Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Abyei, kinachojulikana kama UNISFA, kilirekodi matukio 196 ya usalama yaliyosababisha vifo 58 na majeruhi 69. Aliongeza kuwa idadi hiyo inaashiria "kuongezeka" ikilinganishwa na matukio ya hapo awali mwaka uliopita.

Pia alisisitiza “umuhimu” wa kuteuliwa kwa naibu mkuu wa vikosi hivyo vya UNISFA ambaye si mwanajeshi, huku kukiwa na changamoto za operesheni.

Licha ya hali mbaya eneo hilo, Pobee alisema UNISFA imeendelea kujadiliana na jamii za maeneo hayo, kushika doria na kufanya operesheni kwa lengo la kuwalinda raia na kuepusha vurugu.

"Abyei bado iko kwenye ati ati. UNISFA inaendelea kulinda raia na kuepusha vurugu, lakini haiwezi kuwa mbadala wa kutafuta suluhu," alisema.

UNISFA ilianza majukumu 2011 baada ya vurugu kuzidi katika eneo hilo lenye utajiri mkubwa wa mafuta.

CHANZO:AA