| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
Uturuki yalaumu mashambulizi ya Boko Haram yaliyowaua wanajeshi 23 Chad
Boko Haram, kundi la kigaidi lililoko Nigeria, limekuwa likishambulia maeneo ya Chad yaliyoko karibu na Ziwa Chad katika vurugu zao kwenye kanda.
Uturuki yalaumu mashambulizi ya Boko Haram yaliyowaua wanajeshi 23 Chad
Wanajeshi 23 wa Chad waliuawa na 26 kujeruhiwa katika makabiliano hayo. / Reuters

Uturuki imeshtumu mashambulizi ya Boko Haram katika kambi ya kijeshi ya Chad kwenye mkoa wa Ziwa Chad ambayo yalisababisha vifo vya wanajeshi wasiopungua 23.

“Tunashtumu mashambulizi ya kigaidi kwenye kambi ya kijeshi katika mkoa wa Ziwa Chad ,” wizara ya mambo ya nje ya Uturuki ilisema katika taarifa siku ya Jumatano.

“Tunawaombea rehema za Mungu wanajeshi waliouawa katika shambulizi hilo la kikatili na kutoa rambirambi zetu kwa familia zao na watu wa Chad,” taarifa hiyo ilisema.

Wizara hiyo pia ilisisitiza kuhusu msaada wa Uturuki kwa Chad katika makabiliano yake dhidi ya ugaidi.

Vikosi vya Chad vilikabiliana na wapiganaji wa Boko Haram wakati kundi hilo la kigaidi liliposhambulia kambi ya jeshi kwenye kisiwa cha Barka Tolorom mkoa wa Ziwa Chad, jeshi lilisema siku ya Jumatano.

Lilieleza kuwa "idadi kubwa" ya wapiganaji hao ilikatwa makali na silaha kupatikana, huku msako ukiendelea. Wanajeshi 23 wa Chad waliuawa na 26 kujeruhiwa katika makabiliano hayo.

‘Hali sasa ni shwari’

Jeshi limesisitiza kuhusu dhamira yake ya kukabiliana na magaidi na kuhakikishia raia wa Chad kuwa "hali sasa ni shwari."

"Kwa mara nyingine, magaidi wa Boko Haram walishambulia usiku, shambulio la kioga katika kambi yetu ya kijeshi ya Barka Tolorom, mkoa wa Ziwa Chad," Rais Mahamat Idriss Deby Itno alisema kwenye mtandao wa Facebook.

"Imekabiliwa na ukatili, lakini Chad bado iko imara, ina umoja na haitetereki. Tutaendelea na vita hivi tukiwa na dhamira thabiti hadi tutakapomaliza kabisa tishio hili."

Boko Haram, kundi la kigaidi lililoko Nigeria, limekuwa likishambulia maeneo ya Chad yaliyoko karibu na Ziwa Chad katika vurugu zao kwenye kanda.

Jeshi la Chad limekuwa mstari wa mbele katika juhudi za mataifa kadhaa kukabiliana na kundi hilo eneo la Ziwa Chad, ambapo mashambulizi yamesababisha mauaji ya watu wengi pande zote mbili katika miaka ya hivi karibuni.

CHANZO:TRT World