Afrika Kusini ilijitetea Jumatano dhidi ya madai ya ubaguzi baada ya maandamano kuhusu wahamiaji wasio rasmi na kusema kuwa mataifa ya Afrika yanatakiwa kuangazia masuala kama ya usalama yanayofanya watu wake kuondoka nchini.
Kumekuwa na maandamano kadhaa dhidi ya raia wa kigeni katika wiki za hivi karibuni kwenye taifa liloimarika zaidi kiviwanda barani Afrika, kukiwa na madai ya kushambulia raia wa kigeni, jambo lilofanya Nigeria na Ghana kueleza wasiwasi wao.
"Raia wa Afrika Kusini siyo wabaguzi," msemaji wa rais Vincent Magwenya aliwaambia waandishi wa habari. "Kinachotokea ni maandamano katika sehemu chache, ambayo yanakubaliwa katika mfumo wetu wa katiba."
Katika maandamano mengine siku ya Jumatano, mamia ya watu waliandamana katika mji wa mashariki wa Durban na vituo vingine wakitaka serikali ichukue hatua dhidi ya wahamiaji wasio na hati rasmi wanaoendesha biashara kama maduka madogo.
'Bara la Afrika linahitaji kushirikiana': Marais Ramaphosa, Chapo
Maandamano katika miezi iliopita pia yaliwaondoa wagonjwa wa kigeni wasio na hati rasmi katika zahanati na hospitali za Afrika Kusini.
Katika mazungumzo siku ya Jumanne, Rais wa Msumbiji Daniel Chapo na Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa walikubaliana kuwa "bara la Afrika linahitaji kushirikiana kukabiliana na masuala hayo ambayo yamesababisha viwango hivi vya uhamiaji", msemaji alisema.
Haya ni pamoja na "mizozo, masuala ya ukosefu wa usalama, na maeneo mengine... serikali kushindwa kuhudumia watu wake jambo linalofanya watu kuhama kwa idadi kubwa na kutafuta hifadhi maeneo mengine barani, ikiwemo Afrika Kusini."
Watu wanatakiwa "wawe tayari kujadiliana kuhusu masuala haya na sababu za watu kutaka kuondoka nchi walikozaliwa na kutafuta hifadhi sehemu zingine", Magwenya alisema.




















