| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
Rais wa DRC asema yuko tayari kugombea muhula wa tatu 'kama wananchi watataka'
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Felix Tshisekedi amesema yuko tayari kugombea muhula wa tatu iwapo wananchi wataidhinisha pendekezo hilo.
Rais wa DRC asema yuko tayari kugombea muhula wa tatu 'kama wananchi watataka'
Katiba ya DRC inaruhusu rais kugombea mihula miwili ya miaka mitano mitano, kubadilisha hili kunahitaji marekebisho ya katiba. / Reuters

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Felix Tshisekedi anasema yuko tayari kugombea kwa muhula wa tatu.

Tshisekedi pia anasema mapigano mashariki mwa nchi yanaweza kufanya iwe vigumu kwa uchaguzi wa urais kufanyika kama ilivyopangwa 2028.

"Sijaomba kuchaguliwa kwa muhula wa tatu, lakini kama wananchi wanataka niendelee muhula wa tatu, nitakubali," Tshisekedi aliwaambia waandishi wa habari siku ya Jumatano, akijibu swali kuhusu mapendekezo ya hivi karibuni yaliyowasilishwa na washirika wake kutaka kuifanyia katiba marekebisho.

Katiba ya sasa ya DRC rais anaruhusiwa kugombea mihula miwili pekee. Tshisekedi anasema mabadiliko yoyote yatahitaji marekebisho ya katiba yatakayoidhinishwa na kura ya maamuzi.

Wito wa mabadiliko ya katiba

Tshisekedi, mtoto wa aliyekuwa mwanasiasa nguli wa upinzani Etienne Tshisekedi, alichaguliwa tena Disemba 2023 kwa muhula wa pili.

Alileta wazo hilo la mabadiliko ya katiba kwa mara ya kwanza mwishoni mwa 2024, akieleza kuwa sheria ya sasa kwa sehemu kubwa iliandikwa na wataalamu wa sheria wa kigeni na inahitaji kufanyiwa mabadiliko.

Wito wa kufanyiwa marekebisho ya katiba umeongezeka katika wiki za hivi karibuni. Mwezi Aprili, Andre Mbata, katibu mkuu wa muungano wa Sacred Union, aliviomba vyama vya siasa, makundi ya kiraia, mashirika ya kidini, vyama vya wafanyakazi na wataalamu wa sheria kuwasilisha mapendekezo.

Mbata anasema tume ya wataalamu itaundwa baada ya Mei 20 kutathmini mapendekezo, kabla ya kuwasilisha kwa rais.

CHANZO:TRT Afrika Swahili