Mtu aliyekuwa na bunduki alishambulia waombolezaji waliokuwa wanaondoka kwenye msiba wa mwanasiasa mmoja Jumanne usiku nchini Afrika Kusini, na kuwaua watu wasiopungua wawili pamoja na kuwajeruhi wengine watano, polisi wanasema.
Angalau mmoja ya wale waliojeruhiwa katika tukio hilo la mtaa wa Katlehong, kusini mashariki mwa jiji la Johannesburg, alikuwa mtoto, polisi wanasema. Wanasema mshukiwa amekamatwa baada ya kujisalimisha kwa polisi.
Ushambuliaji huo unachungunzwa na kikosi kazi maalum cha mauaji ya kisiasa, Polisi nchini Afrika Kusini imesema katika taarifa.
Vyombo vya habari vya eneo hilo vimeripoti kuwa wawili wa waliouawa walikuwa wanachama wa kundi la vijana la chama cha ANC, chama chenye wawakilishi wengi zaidi katika Bunge la Afrika Kusini.
Kuhusishwa kisiasa
Taarifa hizo pia zinasema msiba huo ulikuwa wa mwanamke ambaye alikuwa mwanasiasa wa eneo hilo wa ANC na ilikuwa ameuawa kwa kupigwa risasi mwezi huu tukio lililohusishwa na siasa.
Polisi hawakuthibitisha utambulisho wa wawili waliouawa na walisema kuwa walikuwa wanahudhuria msiba wa "mwanachama wa chama cha kisiasa."
Afrika Kusini ina matukio mengi ya uhalifu yanayohusisha bunduki, ikiwemo mashambulio ya risasi kati ya makundi hasimu ya kisiasa.
Afrika Kusini itafanya uchaguzi wake wa serikali za mitaa Novemba 4 kuamua vyama gani vitasimamia manispaa za miji.

























