| Swahili
AFRIKA
3 dk kusoma
Afrika Kusini: Maandamano dhidi ya wahamiaji yazuka tena kufuatia uamuzi wa mahakama
Msemaji wa serikali, William Baloyi, alisema vurugu hizo zilichochewa na watu wanaosambaza taarifa za uongo kwa makusudi kuhusu uamuzi uliotolewa na Mahakama ya Katiba mwezi Julai.
Afrika Kusini: Maandamano dhidi ya wahamiaji yazuka tena kufuatia uamuzi wa mahakama
Maandamano yaliongozwa na kundi lililotaka kituo cha wakimbizi kusitisha kushughulikia maombi ya wanaoomba hifadhi. /

Maandamano dhidi ya wahamiaji katika miji miwili ya Afrika Kusini, ikiwemo eneo la Soweto jijini Johannesburg, yaligeuka kuwa vurugu siku ya Alhamisi. Serikali imehusisha machafuko hayo na taarifa za upotoshaji kufuatia uamuzi wa mahakama kuhusu waomba hifadhi.

Katika mji wa pwani wa Durban, ambao pia ulikumbwa na maandamano hayo, mwandishi wa Shirika la Habari la Reuters alishuhudia magari matano yakichomwa moto katikati ya mji. Maduka yanayomilikiwa na raia wa kigeni pia yalivamiwa na kuporwa.

Machafuko hayo yalifuatia maandamano yaliyoongozwa na kundi lililotaka kituo cha wakimbizi kusitisha kushughulikia maombi ya hifadhi.

Katika eneo la Soweto, mwandishi wa Reuters alishuhudia wakazi wakibeba bidhaa za dukani, wakidai kuwa duka hilo lilimilikiwa na raia wa Somalia ambaye walikuwa wamemfukuza eneo hilo. Waporaji walikimbia baada ya polisi kufika eneo hilo.

Msemaji wa serikali, William Baloyi, alisema vurugu hizo zilichochewa na watu wanaosambaza taarifa za uongo kwa makusudi kuhusu uamuzi uliotolewa na Mahakama ya Katiba mwezi Julai.

Mahakama hiyo ya juu zaidi nchini humo iliamua kuwa waomba hifadhi hawawezi kunyimwa fursa ya kutumia mfumo wa maombi ya hifadhi nchini Afrika Kusini kwa sababu za kiutaratibu pekee, kama vile kuingia nchini humo kinyume cha sheria.

Baloyi alisema uamuzi huo umepotoshwa kwa kiasi kikubwa na kusisitiza kuwa hauwapi moja kwa moja wahamiaji wasio na nyaraka hadhi ya ukimbizi, ukaazi wa kudumu au haki nyingine za kisheria.

"Tuna wasiwasi mkubwa kuhusu kinachoendelea sasa," alisema.

Polisi walisema katika taarifa yao kuwa wameongeza idadi ya maafisa katika mji wa Durban, ambako waliripoti kuwa angalau magari 14 yalichomwa moto. Nyumba ya wageni na ghala pia vilichomwa moto kwa sehemu.

Afisa mwandamizi wa polisi, Luteni Jenerali Puleng Dimpane, aliwaambia waandishi wa habari katika mkutano uliofanyika Soweto kwamba wahusika wa vitendo vya vurugu na uharibifu watatambuliwa na kuchunguzwa, na wale watakaopatikana na ushahidi wa kutosha watafunguliwa mashtaka na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Dimpane alisema magari 10 yalikuwa yamechomwa moto katika eneo la Soweto, lakini hali ilikuwa imedhibitiwa.

Afrika Kusini imekumbwa na miezi kadhaa ya maandamano dhidi ya wahamiaji mwaka huu, hali iliyosababisha ukosoaji kutoka jumuiya ya kimataifa.

Baadhi ya maandamano hayo yamegeuka kuwa vurugu na uporaji, huku maelfu ya raia wa nchi nyingine za Afrika wakilazimika kuondoka nchini humo.

Wahamiaji mara nyingi hutuhumiwa kuchukua nafasi za ajira za wenyeji, kuchochea uhalifu na kuongeza mzigo katika huduma za umma. Hata hivyo, wanasayansi wa jamii wanasema madai hayo hayana ushahidi wowote.

Miaka 30 baada ya kumalizika kwa mfumo wa ubaguzi wa rangi wa ‘apartheid’, Afrika Kusini bado inakabiliwa na pengo kubwa la kiuchumi na kijamii. Takribani theluthi moja ya watu wake hawana ajira.

Licha ya changamoto hizo, Afrika Kusini bado ndiyo yenye uchumi mkubwa zaidi barani Afrika na inaendelea kuvutia wahamiaji kutoka mataifa mbalimbali.

CHANZO:Reuters