Ujasiri wa wanaojitolea kwa majaribio ya tiba na chanjo
AFRIKA
5 dk kusoma
Ujasiri wa wanaojitolea kwa majaribio ya tiba na chanjoNchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), wanaojitolea katika majaribio ya tiba ya Ebola wana matumaini kuwa kushiriki kwao kutawasaidia wanasayansi kupiga hatua katika kutafuta njia ya kukabiliana na ugonjwa huo.
Nchini DRC, majaribio ya kimatibabu ni mchango muhimu katika utafiti unaoweza kutoa matumaini kwa wengine. / reuters

Na Dayo Yussuf

Amina, ambaye jina lake halisi tumelibana ili asitambuliwe, aliamua kushiriki katika jaribio la kimatibabu la tiba mpya ya Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Kwake yeye, uamuzi huo ulikuwa wa kibinafsi. Alikuwa amempoteza mjomba wake kutokana na virusi hivyo hatari, na tukio hilo lilimfanya awe na azma ya kufanya jambo ambalo lingeweza kuwasaidia wengine wanaokabiliwa na tishio hilo.

"Kilichonichochea kushiriki ni kifo cha mjomba wangu. Alipofariki, majibu ya vipimo yalionyesha kuwa ana maambukizi (ya Ebola). Kwa kuwa nilikuwa nimewahi kutangamana naye, jambo hili lilinichochea kuja hapa."

Amina ni miongoni mwa watu 250 waliojitolea katika utafiti huo wa tiba ya majaribio kwa matumaini kuwa inaweza kusaidia kupambana na ugonjwa ambao umesababisha vifo vya maelfu ya watu.

Vigezo vya WHO

Kwa walijiotolea kama yeye, uamuzi huo ni zaidi ya uwezekano wa kupata matibabu mapya. Pia unahusu kuchangia katika utafiti ambao unaweza kuwapa wengine matumaini.

Lakini ni nini kinachohitajika ili chanjo au dawa mpya ifikie hatua ya kufanyiwa majaribio kwa binadamu? Na wanasayansi huhakikisha vipi kuwa watu wanaojitolea wanalindwa?

Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), mchakato huo huanza muda mrefu kabla ya mtu wa kwanza kusajiliwa.

Awali, wanasayansi hufanya utafiti wa maabara ili kubaini iwapo matibabu au chanjo inayokusudiwa ina msingi thabiti wa kisayansi.

"Tunachofanya kwanza kama wanasayansi ni kujaribu pendekezo hilo maabara; hii inaweza kufanyika kwa kutumia seli. Tunaangalia kwa mfano, kama ni virusi—iwapo dawa hiyo inaweza kuzuia virusi hivyo kuzaliana," anasema Dkt. Reena Doshi, mtaalamu wa magonjwa ya mlipuko katika Shirika la Afya Duniani. "Iwapo chanjo inaweza kuzuia virusi kuzaliana, au iwapo inachochea uzalishaji wa kingamwili na kama kingamwili hizo zinaweza kuvizuia virusi hivyo," aliiambia TRT Afrika.

Hii inajulikana kama utafiti wa awali wa kimatibabu (pre-clinical research). Inawasaidia watafiti kubaini iwapo wazo fulani linastahili kufanyiwa utafiti zaidi kabla ya kufikiria kulijaribu kwa binadamu.

Kamati ya maadili

Hata hivyo, matokeo ya maabara yanayoonyesha matumaini pekee hayatoshi kuanzisha majaribio ya kimatibabu.

Ni lazima watafiti kwanza waandae mpango wa kina wa jaribio hilo, wakielezea kile wanachotaka kubaini, jinsi utafiti utakavyofanywa, hatari na faida zinazoweza kujitokeza, pamoja na hatua zitakazochukuliwa kulinda wanaojitolea.

Pia, ni lazima kamati huru ya maadili ipitie na kuidhinisha utafiti huo.

Hata baada ya hatua hizi, si kila mtu anayejitolea ataruhusiwa kushiriki.
Watafiti huweka vigezo maalum vya kustahiki kushiriki kulingana na lengo la utafiti.

"Kuna kanuni zilizo wazi wakati wa kuandaa mpango wa utafiti kuhusu nani anayetakiwa kushiriki. Hii inaweza kuhusisha umri maalum, kama tunatafuta suluhisho kwa ajili ya watoto, au hali maalum ya kiafya, kwa mfano wagonjwa wa saratani. Kwa kweli inategemea aina ya matibabu, iwe ni dawa au chanjo, na mambo mengine mengi. Pia, kujitolea hakumaanishi moja kwa moja kuwa utakubaliwa kushiriki, kwa sababu lazima utimize vigezo hivyo vilivyowekwa awali," Dkt. Doshi anaiambia TRT Afrika.

Kwanini majaribio yanafanyika Afrika?

Hatua hizi za kinga ni muhimu sana wakati jaribio linahusisha ugonjwa kama vile Ebola, ambao unaweza kusababisha ugonjwa hatari na hata kifo.

Pia zinasaidia kujibu maswali kuhusu sababu zinazofanya majaribio fulani ya kimatibabu kufanyika katika nchi za Afrika, na iwapo rangi ya ngozi ina nafasi katika kuamua nani anayehusishwa.

Dkt. Doshi anasema rangi haitakiwi kuwa kigezo cha kustahiki kushiriki. Badala yake, eneo na kiwango cha mlipuko wa ugonjwa vinaweza kuathiri mahali ambapo watafiti wanahitaji kufanyia tafiti zao.

"Rangi haipaswi kuwa na ushawishi wowote katika jaribio hilo," anaeleza. "Changamoto iliyopo katika baadhi ya magonjwa haya adimu, kwa mfano Ebola na BVD, ni kuwepo kwa aina fulani ya virusi vya Ebola. Huu ni mlipuko wa tatu tu tunaoufahamu, na milipuko hiyo yote imetokea barani Afrika. Hivyo, wakati mwingine tunalazimika kufanyia majaribio ya dawa mpya na chanjo mpya katika maeneo yenye maambukizi au mlipuko halisi wa ugonjwa huo; katika hali hii, ni miongoni mwa jamii za Kiafrika ambapo ugonjwa huo umejikita, na hasa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC)."

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), wanaojitolea katika majaribio ya tiba ya Ebola wana matumaini kuwa kushiriki kwao kutawasaidia wanasayansi kupiga hatua katika kutafuta njia ya kukabiliana na ugonjwa huo.

Majaribio ni kubahatisha

Jacques Zawadi, daktari mtafiti anayehusika na jaribio la dawa ya EBO-PEP, anasema kwa watu kujitolea kumeleta matumaini.

“Wanaojitolea kwa ujumla wanaonesha kuridhika, kwa sababu jambo hili linatoa matumaini. Kugundua dawa ya kutibu ugonjwa ambao hauna tiba kunaleta matumaini. Wengi wanafurahia kuwa pamoja na sisi na kunufaika na matibabu haya, ingawa bado ni ya majaribio.”

Hata hivyo, majaribio ya kimatibabu hayatoi uhakika wa kufanikiwa. Matibabu ya majaribio yanaweza kuonekana kutofaa au kufichua hatari ambazo hazikujulikana hapo awali. Lengo la utafiti huo ni kubaini, kupitia tafiti zinazofuatiliwa kwa uangalifu, iwapo matibabu hayo ni salama na yanafaa.

Kushiriki katika majaribio ya kimatibabu kwa binadamu bado ni hatua muhimu katika utafiti wa matibabu, lakini watu wengi bado wanahofia kujitolea.

Lakini kwa Amina na wengine kama yeye, uamuzi huo ulitokana na tukio la kuhuzunisha lililomgusa binafsi. Yale ambayo watafiti wanajifunza kutokana na kujitolea kwao yanaweza kusaidia kuandaa mikakati ya kukabiliana na milipuko ya magonjwa hayo baadaye.

CHANZO:TRT Afrika Hausa