Maafisa wa usalama nchini Marekani wamevamia nyumba ya Mwakilishi wa chama cha Democratic Ilhan Omar ya jijini Washington, DC mapema siku ya Jumatatu kwa lengo la uchunguzi kuhusu taarifa zake za uhamiaji, Shirika la habari la Marekani la Fox News limeripoti.
Maafisa wa serikali walitekeleza oparesheni iliyoidhinishwa na mahakama saa kumi na mbili asubuhi, wakiangazia udanganyifu wa nyaraka za uhamiaji za Mwakilishi huyo alipokuwa mdogo. Ilhan Omar mwenye umri wa miaka 44 alizaliwa nchini Somalia.
"Uchunguzi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ni utekelezaji wa agizo la mahakama lililopatikana kwa ombi la Wizara ya Haki," msemaji wa wizara hiyo aliliambia shirika la Fox News, akieleza kuwa msako huo ni sehemu ya uchunguzi wa serikali unaoendelea.
Idara ya Uchunguzi ya Wizara ya Mambo ya Ndani iliongoza oparesheni hiyo.
Omar au ofisi yake ya Uwakilishi haijatoa taarifa kuhusu msako huo wa asubuhi.
Hatua hii inafuata matamshi ya Mkuu wa Uhamiaji wa Marekani Tom Homan, ambaye alikiri hadharani kuhusu uchunguzi wa uhalifu kuhusu Mwakilishi huyo wa Minnesota katikati mwa mwezi Septemba.
Kumekuwa na hali ya taharuki kati ya Omar na Rais wa Marekani Donald Trump kuhusu utekelezaji wa sheria ya Uhamiaji na Forodha Minnesota.
Familia ya Omar iliingia nchini Marekani 1995, yeye akiwa kijana, baada ya kupata hifadhi ya kisiasa.




















