Kuelekea Uchaguzi Mkuu 2027 Kenya
AFRIKA
6 dk kusoma
Kuelekea Uchaguzi Mkuu 2027 KenyaTayari joto la uchaguzi limeanza kuonekana nchini humo huku wanasiasa wakipimana nguvu kupitia mikutano ya hadhara, japo kipindi rasmi cha kampeni hakijaanza.
Kenya inafanya Uchaguzi Mkuu Agosti 10, 2027.

Kenya inajiandaa kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu ulioratibiwa kufanyika tarehe 10 Agosti 2027.

Tayari joto la uchaguzi limeanza kuonekana nchini humo huku wanasiasa wakipimana nguvu kupitia mikutano ya hadhara, japo kipindi rasmi cha kampeni hakijaanza.

Rais William Ruto, rasmi ametangaza nia ya kuomba tena ridhaa ya wananchi kuliongoza taifa hilo kwa muhula wa pili.

Rais Ruto, anaamini kuwa huenda akapewa fursa hiyo tena kutokana na miradi kadhaa ya maendeleo ambayo ameianzisha katika kipindi chake cha kwanza.

‘‘Mimi nikichukua kama Rais 2022 uwekezaji kutoka nje ambayo ilikuwa imekuja Kenya ni Dola bilioni 1.6 mwaka uliopita 2025 ilikuwa imefika Dola bilioni 3.1’’, anaeleza Rais Ruto.

Baadhi ya miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa nyumba za bei nafuu ambao umeleta ajira na pengine unafuu kwa baadhi ya wananchi. Rais akisema tangu kuanzishwa kwake 2022, umeleta ajira zaidi ya milioni 1. 

Kulingana na ilani ya chama chake na ahadi ni kujenga nyumba katika ya 200,000 na 250,000 kwa mwaka katika miji mbalimbali.

Akieleza kuwa lengo ni kutimiza nyumba 1,000,000 katika kipindi cha zaidi ya miaka mitano. Kufikia mwishoni mwa mwaka 2025, idadi ya ujenzi wa nyumba 200,000 ilikuwa haijafikiwa.

Pia kuna huduma ya afya kwa wote maarufu SHA, ingawa bima hii imekuwa ikikosolewa na baadhi ya watu kuwa haifikii wote. 

Ujenzi wa miundombinu katika baadhi ya maeneo ikiwemo mradi wa reli ya mizigo, na uzinduzi wa ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta mjini Lamu, pwani ya Kenya.

Kupitia miradi hii, Rais Ruto, anahisi Wakenya kupitia sanduku la kura, watampa muhula wa pili.

‘‘Mwekezaji hataki kusumbuliwa, hataki masharti, anataka motisha, mwekezaji anataka vile serikali itamrahisishia mambo, siyo serikali kuipatia ati mwekezaji masharti ‘‘, anaongeza Rais Ruto  

Kauli mbiu ya ‘Wantam’

Mafanikio ya Rais Ruto, yanaweza kuwa ni makubwa, lakini bado anakabiliwa na upinzani mkubwa nchini mwake.

Wapinzani wake wanadai kuwa Rais Ruto, ameshindwa kusimamia mabadiliko ya kweli ya kiuchumi kwa lengo la kunufaisha mwananchi wa kawaida.

Baadhi ya waliojitokeza kumpinga, wametumia kigezo hicho, na kuonesha nia ya kutaka kumuondoa madarakani.

Mahasimu wakuu

Wanaoonekana kuwa mstari wa mbele kumpinga Rais Ruto, ni aliyekuwa Naibu wake, Rigathi Gachagua.

Tangu alipoondolewa katika nafasi hiyo, Riggy G amekuwa mwiba katika uongozi wa Rais Ruto.

Mara nyingi, amesikika hadharani akiikosoa serikali ya Rais Ruto kwa tuhuma mbalimbali.

Gachagua anasema serikali ilioko sasa inashindwa kutambua vipaumbele vya wananchi.

‘‘Ukiona sadaka imeenda chini ujue uchumi umezoroteka..sasa nimeona huyu waziri wa Ruto anaitwa Mbadi ati mtaalamu anasema ati uchumi inaendelea vizuri ati watu wanakunywa soda zaidi’’, anaeleza Gachagua.

Jinamizi la Gen Z

Jinamizi la maandamano ya Gen Z ya Juni 2024 bado linaendelea kuiandama serikali ya Rais Ruto.

Juni 2024, kulikuwepo na moja ya maandamano makubwa katika historia ya Kenya.

Maelfu ya vijana, katika miji mbalimbali, ikiwemo mji mkuu wa Nairobi waliingia mitaani, kupinga kile walichokiita Muswada tata wa Fedha.

Waliishinikiza serikali kuuondoa Muswada huo, wakidai kuwa ulikuwa na lengo la kuwakandamiza wananchi.

Serikali nayo, kupitia maafisa wa usalama na ulinzi, ilionekana kutumia nguvu zaidi kukabiliana na waandamanaji.

‘‘Nimesema askari mwenye atasumbuliwa ati anapelekwa kortini kwa sababu anatumia bunduki kujichunga ama kuchunga kituo cha polisi ama kuchunga bunge ama kuchunga ofii ya serikali  kortini ama wapi, mtu akijaribu kwanza..hawezi kwa sababu hatutatoa ushirikiano.’’ Anasema Waziri wa Mambo wa Ndani wa Kenya, Kipchumba Murkomen.

Msimamo huo wa serikali, ulileta madhara makubwa, watu wasiopungua 60 waliuawa na mamia wengine kujeruhiwa, mali ziliharibiwa na hasara kutokana na watu kusitisha biashara zao. 

Vijana walijawa na hasira.

Mapambano yakaongezeka kati yao na polisi. Pole pole, sauti ya na muelekeo wa Gen Z ikaanza kubadilika.

Ikawa sio madai tena ya kupinga Muswada tata wa Fedha, bali ni sauti ya kumtaka Rais Ruto kuondoka madarakani.

Miaka miwili baadaye, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya Kipchumba Murkomen amekiri hadharani kuwa serikali haikulishughulikia suala hilo vyema.

‘‘Taifa lililo salama siyo lile ambalo serikali inajuwa kila kitu, ni lile ambalo serikali inakuwa sikivu na inajifunza na kuchukua hatua.’’ Murkomen anakiri.

Lakini maji yakishamwagika, kuzoleka tena sio rahisi.

Kwa Gen Z imekuwa ni kama kidonda kilichokataa kupona.

Na kutimuliwa kwa Katibu Mkuu katika chama cha ODM Edwin Sifuna kukatoa msukumo wa kumuona kama kiongozi mbadala atakayewakilisha maslahi yao.

‘‘Ukiangalia katika maeneo yote Kenya Linda Mwananchi ndiyo kusema kwa sasa kwa sababu tumewapa wananchi kipaumbele’’, Seneta wa Nairobi ambaye ni mmoja wa vinara wa vuguvugu la ‘Linda Mwananchi’’ Edwin Sifuna anasema.

Edwin Sifuna

Aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa chama cha ODM, Chama hicho ndicho kilichokuwa cha aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Kenya Raila Odinga. Nyota yake ilianza kuvutia wengi, pale tu alipotimuliwa katika chama hicho huku vijana wakionesha kuvutiwa nae.

Ingawa hajaelezea kwa undani sera yake, amevutia wengi tu kwa kauli mbiu yake ya 'Wantam' ya kutaka kumuondoa Rais Ruto madarakani.

Katika siku za hivi karibuni, ameonekana kuwa na mvuto wa kweli.

Maelfu ya vijana wamekuwa wakivutiwa nae, kiasi cha kutetemesha ngome za wanasiasa wakongwe.

Ni hivi majuzi ambapo wanachama wa vuguvugu la Linda Mwananchi walimpendekeza awe mgombea wao wa Urais kwenye Uchaguzi Mkuu 2027 huku wanasiasa wengine, tayari wakionesha nia ya kufanya kazi naye.

‘‘Na niko tayari…kama tumepiga hesabu zetu na kuona kuwa Sifuna ndiyo atapeleka hii mtu nyumbani mapema..ni sawa…na hakuna tatizo hata mimi Riggy G naweza kuwa naibu wa Sifuna..kwani iko makosa gani?’’, alieleza aliyekuwa Naibu wa Rais, Rigathi Gachagua.

Lakini, siasa siku zote hazitabiriki, na muda uliopo kuanzia sasa hadi Agosti mwakani, chochote kinaweza kutokea. 

‘‘Hiyo mambo sijui familia maarufu, ‘hustler’ imewaletea nini? Imewaletea nini? Sasa mkuje muambiwe siasa nyingine ya ukabila itawaletea nini isipokuwa shida? msikubali, anasema Rais Mstaafu wa Kenya,Uhuru Kenyatta.

Hivyo, swali lililopo, ni iwapo nyota ya Sifuna itaendelea kung'aa au kufifia?

‘‘Ruto mwenyewe tayari ameanza kufanya miradi, barabara ya Mau Summit itakamilika, inabidi uoneshe watu kuwa si barabara pekee kama ambavyo Sifuna anasema, lakini hata wakati Sifuna akisema mambo ya kuvutia, watu wengi wanauliza, wengine wananipigia simu wananiambia ambia Sifuna aache mchezo, watu hawakuli hiyo haki za binadamu, hiyo sheria’’. mchambuzi wa siasa Herman Manyora anaeleza.

Upinzani-Unatakiwa kufanya nini kumuondoa Ruto? na Rais Ruto anatakiwa kufanya nini kuusambaratisha upinzani?

Mchambuzi wa siasa Profesa Peter Kagwanja anasema inawezekana kumshinda Rais Ruto kama kutakuwa na mkakati.

‘‘William Ruto anaweza kushindwa na siyo kushindwa tu bali kushindwa hadi watu wamsahau na tuendelee na maisha yetu kama taifa. Inawezekana, kwa sababu tumeshawahi kufanya hivyo hapo awali.’’ Profesa Peter Kagwanja anasisitiza.

Muda unakwenda mbele haurudi nyuma na Agosti 10 mwakani ndiyo itakuwa msema kweli wakati raia wa Kenya watakapojitokeza kutimiza haki yao ya kimsingi na kikatiba, kupiga kura.

 



 






CHANZO:TRT Afrika Swahili