Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed, amezindua rasmi kiwanda cha kwanza cha kusafisha dhahabu na madini ya thamani nchini humo.
Kiwanda hicho, kilichopo katika ukanda maalum wa kiuchumi wa Bole Lemi karibu na Addis Ababa, kinalenga kuifanya Ethiopia kuwa kitovu kikubwa cha usafishaji na uongezaji thamani wa madini barani Afrika.
Mradi huo, wenye thamani ya Dola milioni 50, ni uwekezaji wa pamoja katika ya kampuni ya serikali ya Ethiopian Investment Holdings, yenye umiliki wa asilimia 51, na kampuni ya kimataifa ya Sam Precious Metals, itakayomiliki asilimia 49 za hisa hizo.
Kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kusafisha zaidi ya tani 600 za madini ya thamani kwa mwaka, ikiwemo dhahabu na fedha, kwa lengo la kusitisha usafirishaji wa nje wa dhahabu ghafi kwa ajili ya kuongezewa thamani.
Hatua hiyo, inakuja wiki moja baada ya Burkina Faso, kuzindua kiwanda cha kusafisha dhahabu, chenye uwezo wa kusafisha takribani tani 164 za dhahabu kwa mwaka katika awamu ya awali, huku kukiwa na mipango ya kuongeza uwezo huo kufikia tani 515 kwa mwaka.


















