Jamhuri ya Uturuki ya Kupro Kaskazini (TRNC) siku ya Alhamisi ilishtumu Umoja wa Ulaya kwa kwenda kinyume na ahadi zake za zamani za kumaliza kuwatenga watu wa Kupro ya Uturuki na juhudi za “kuimarisha ushirikiano” na “kuendeleza majadiliano,” ambapo TRNC imetaja kama jaribio la “kuhadaa” kuhusu hatua zilizopigwa.
Wizara ya Mambo ya Nje ya TRNC inasema maelekezo ya barua ya Tume hayakuangazia uhalisia katika kisiwa hicho, ikishtumu EU kwa kuendeleza msimamo wa “upendeleo na kukosa msingi” kuhusu suala la Kupro.
Wizara hiyo inasema kwa miaka mingi Waturuki wa Kupro wamekuwa wakiishi chini ya kile walichokieleza kuwa kutengwa pamoja na vikwazo ikiwa ni ukiukwaji wa sheria ya kimataifa na haki za binadamu.
Ilisema kuwa vikwazo katika maeneo ikiwemo elimu na michezo mpaka utamaduni na masuala ya uchumi vimekiuka haki za kimsingi za Waturuki wa Kupro.
Taarifa hiyo pia inashtumu EU kwa kuendeleza “msimamo usio wa haki” kuhusu kisiwa hicho na kurubuniwa kwa kura ya turufu ya upande wa Kupro ya Ugiriki.
“Ukweli uko wazi : watu wa TRNC bado wanakabiliwa na kutengwa huku EU na jamii ya kimataifa ikiona hili,” taarifa ilisema.
EU ‘haina nia’ ya kuachana na hali ya kutengwa
Taarifa ya TRNC inaeleza kuwa yaliyoelezwa na Tume ya Ulaya kulingana na maamuzi ya Baraza la Ulaya ya 2004 yenye lengo la kumaliza kutengwa kwa Kupro ya Uturuki, pamoja na madai kuhusu “kuimarisha ushirikiano” na “kuendeleza majadiliano,” ni “jaribio la kutoa taswira ya kupotosha.”
“EU haijachukua hatua madhubuti, na imeonesha kuwa hakuna mtazamo wa kweli, utashi wa kisiasa au dira ya kuondoa vikwazo visivyo vya haki kwa watu wa Kupro ya Uturuki pamoja na vikwazo vinavyowekwa na upande wa Kupro ya Ugiriki.
"EU, ambayo inaunga mkono uongozi wa Kupro ya Ugiriki ambao pia unazuia vijana wetu na wanamichezo kushirikiana na watu wengine duniani, ndiyo wanaokingia kifua hali ilivyo kwa sasa katika kisiwa hicho," iliongeza.
“Hatuwezi kuuamini Umoja wa Ulaya na yule anayejiita kuwa mwakilishi wake, (Makamu wa Rais wa Tume ya Ulaya na Mjumbe Maalum wa EU wa Kupro) Raffaele Fitto, ambaye anabeza utashi, usawa, na hadhi sawa ya kimataifa kwa watu wa Kupro ya Uturuki na kubadilisha uhalisia wa kisiwa hicho kupitia taarifa zenye upendeleo, barua na taarifa.”
Taarifa hiyo inasema watu wa Kupro ya Uturuki na TRNC wataendelea na harakati zao chini ya mfumo wao wa taifa, na kuungwa mkono kwa dhati na Jamhuri ya Uturuki, na itaendelea kutetea haki kwa misingi ya usawa licha ya vikwazo vyote na majaribio ya kuleta pingamizi.
“TRNC haitokubali mbinu hizi zisizo na msingi na zenye lengo la kuficha mazingira ya yasiyokuwa ya haki kwa kisiwa hicho. Lazima jamii ya kimataifa ifahamu jambo moja la kweli: hadi pale vikwazo vyote visivyo na msingi vilivyowekwa kwa watu wa Kupro ya Uturuki viondolewe vyote, na tupate usawa na hadhi itambulike kimataifa, azimio la EU la ‘nia njema’ halina msingi wowote kwetu.
“Wakati huo huo, si rahisi kuelewa upotoshaji unaofanyika kwa umma na vyombo vya habari kuwa kuna hatua zilizopigwa na EU kuhusu kutengwa kwa eneo hilo. EU siyo haiwezi kuondoa kutengwa kwa watu wa Kupro ya Uturuki, hata kuonesha nia ya kupatikana kwa afuweni haina.”
Tatizo la miongo kadhaa
Kisiwa hicho kimekuwa katika hali ya mvutano kwa miongo kadhaa kati ya Kupro ya Ugiriki na Kupro ya Uturuki.
Mwaka 1974, mapinduzi ya Kupro ya Ugiriki yaliyokuwa na lengo la kumega kisiwa hicho kuwa sehemu ya Ugiriki yalikabiliwa kijeshi na Uturuki kama mdhamini wa kulinda watu wa Kupro ya Uturuki wasiteswe na kufanyiwa vurugu. Matokeo yake, TRNC ikaanzishwa mwaka 1983.
Kumekuwa na michakato mbali mbali ya amani katika miaka ya hivi karibuni, ikiwemo ule uliotibuka wa Uswisi wa mwaka 2017 chini ya mataifa wadhamini ya Uturuki, Ugiriki na Uingereza.
Kupro ya Kusini inayosimamiwa na Ugiriki ilijiunga na Umoja wa Ulaya mwaka 2004, mwaka huo huo ambao Kupro ya Ugiriki ilipinga mpango wa Umoja wa Mataifa kumaliza mgogoro huo wa muda mrefu.




















