Serikali ya Mauritius imefunga shule katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo kufuatia machafuko yaliyozuka usiku wa kuamkia Jumanne, baada ya polisi kumpiga risasi msichana.
Sajenti wa polisi amefunguliwa mashtaka kuhusiana na tukio la kumpiga risasi Élodie Thomas, mwenye umri wa miaka 27, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya nchini humo.
Hata hivyo, taarifa hizo hazikueleza kwa kina kilichosababisha tukio hilo.
Thomas alijeruhiwa kwa risasi Ijumaa usiku alipokuwa kwenye gari akirudi nyumbani kutoka kazini, katika eneo la makazi lililopo kusini mwa mji mkuu wa nchi hiyo.
Waziri wa Afya, Anil Bachoo, alisema Thomas alifanyiwa upasuaji na kutolewa risasi iliyokuwa mwilini mwake.
Uchunguzi wa tukio hilo laendelea
Polisi bado hawajatoa maelezo rasmi kuhusu tukio hilo, lakini wamethibitisha kuwa uchunguzi unaendelea.
Usiku wa Jumatatu, waandamanaji walichoma matairi na kufunga barabara katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo, hali iliyosababisha polisi kupelekwa katika maeneo yaliyoathirika kudhibiti hali ya usalama.
Kutokana na vurugu hizo, mitihani ya tathmini ya wanafunzi iliyopangwa kufanyika Jumanne, Oktoba 13, imeahirishwa hadi tarehe nyingine.
Wizara ya Elimu ilitangaza kuwa shule za chekechea, shule za msingi na sekondari zitafungwa siku nzima ya Jumanne, Oktoba 13.
Aidha, wanafunzi wa vyuo vikuu na taasisi nyingine za elimu ya juu wameelekezwa kuendelea na masomo kwa njia ya mtandao. Mihadhara yote iliyopangwa kufanyika siku hiyo itafanyika kwa njia ya mtandao.
Ofisi ya Waziri Mkuu ilisema hali ya usalama nchini humo imerejea katika hali ya kawaida na kwamba huduma zote za sekta ya umma zitaendelea kutolewa kama kawaida.
Machafuko ya aina hiyo si ya kawaida katika kisiwa hicho kilichopo katika Bahari ya Hindi.
Hata hivyo, Wizara ya Elimu haikutaja tarehe ambayo shule zitafunguliwa tena, ikisema itatoa taarifa zaidi baadaye.





















