Mtu mmoja amepoteza maisha jijini Frankfurt nchini Ujerumani, baada ya kuugua ugonjwa wa Malaria.
“Mgonjwa huyo ni kati ya wagonjwa wawili walioripotiwa mapema wiki huu katika wilaya ya Schwanheim, ilisema taarifa iliyotolewa na wilaya hiyo siku ya Alhamisi.
Kulingana na idara ya afya ya wilaya hiyo, watu hao wawili waliugua Malaria mara baada ya kung’atwa na mbu, aliyeingia ndani ya ndege iliyokuwa ikielekea jijini Frankfurt.
Idadi ya watu waliopoteza maisha kwa ugonjwa huo katika eneo hilo, sasa imefikia watatu.
Mwezi uliopita, wafanyakazi sita wa uwanja wa ndege wa Frankfurt waliugua ugonjwa wa Malaria, huku wawili wakipoteza maisha.
Malaria ni ugonjwa hatari unaosababishwa na vimelea vya Plasmodium na kusambazwa kupitia kuumwa na mbu jike aina ya Anopheles.





















