Mamlaka nchini Libya zimekamata shehena ya maelfu ya vidonge vya dawa za kulevya aina ya ecstasy, vilivyowekwa alama ya picha ya kiongozi wa zamani wa nchi hiyo, Muammar Gaddafi. Kwa mujibu wa maafisa wa usalama, vidonge hivyo vilisafirishwa kwa njia ya magendo kutoka Ulaya.
Picha zilizotolewa na chombo cha usalama mjini Tripoli zilionesha magunia yaliyokuwa na vidonge vya rangi ya kahawia, vilivyotengenezwa kwa umbo la kichwa na mabega ya Gaddafi. Tembe hizo zilikuwa na michoro inayoakisi sura yake ya kipekee pamoja na vazi alilokuwa akilitumia.
Kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa Januari, Libya imekuwa kitovu cha usafirishaji wa dawa za kulevya za kutengenezwa viwandani na aina nyinyingine ya mihadarati, ambayo husafirishwa kwenda kwa watumiaji wa ndani na maeneo mengine ya Afrika Kaskazini pamoja na sehemu mbalimbali za bara la Afrika.
Ripoti hiyo, iliyotolewa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC), ilisema magenge ya biashara ya dawa za kulevya yamekuwa yakitumia fursa ya hali ya machafuko nchini humo tangu mwaka 2011.
Kwa mujibu wa taarifa, maafisa wa usalama walipata taarifa kwamba genge moja lilikuwa likipanga kusafirisha dawa hizo kwa njia ya bahari.
Maafisa waliizuia shehena hiyo baada ya kuwasili na kugundua kwamba vidonge hivyo vilikuwa vimefichwa ndani ya gari la kubebea mizigo, taarifa hiyo iliongeza.
"Operesheni hiyo ilifanikisha kukamatwa kwa jumla ya takribani vidonge 100,000 vya 'XTC' (Ecstasy)," taarifa hiyo ilisema, huku idadi ya washukiwa ikiwasilishwa kwa waendesha mashtaka.

















