| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
Mufti Mkuu Tanzania atoa wito kwa Waislamu kufunga siku tatu kuomba kuepushwa na madhara ya El Nino
Mufti Mkuu amewaomba Waislamu kumuomba Mwenyezi Mungu afanye mvua hizo kuwa mvua ya rehema na yenye manufaa kwa jamii, badala ya kuwa chanzo cha adhabu na maafa.
Mufti Mkuu Tanzania atoa wito kwa Waislamu kufunga siku tatu kuomba kuepushwa na madhara ya El Nino
Mufti Mkuu amesema kuna matarajio ya kunyesha kwa mvua kubwa za El Nino katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania. /

Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir bin Ally, amewataka Mashekhe na Waislamu kwa ujumla kufunga kwa siku tatu kuanzia Septemba 10, 2026, huku akiwataka kumuomba Mwenyezi Mungu aepushe taifa na madhara yanayoweza kusababishwa na mvua kubwa zinazotabiriwa.

Akizungumza kuhusu taarifa za Serikali kupitia Idara ya Hali ya Hewa, Mufti Mkuu amesema kuna matarajio ya kunyesha kwa mvua kubwa za El Nino katika maeneo mbalimbali nchini, hivyo ametoa wito kwa viongozi wa dini na Waislamu wote kushiriki katika ibada hiyo ya kufunga na kumuomba Mwenyezi Mungu kuiepusha nchi na majanga.

“Kwa mujibu wa maelezo au taarifa ya Serikali kupitia Idara ya Hali ya Hewa, inatarajiwa kunyesha mvua kubwa ya El Nino kote nchini kwa kiwango kikubwa sana,” amesema.

Kutokana na hali hiyo, Sheikh Dkt. Abubakar amewataka Mashekhe wa mikoa, wilaya na kata, Maimamu, viongozi wa taasisi za Kiislamu pamoja na Waislamu wote kwa ujumla kufunga kwa siku tatu na kutumia siku hizo kumuomba Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Ta’ala kuondoa mabalaa na majanga yanayoweza kujitokeza.

“Nachukua fursa hii kuwataka Mashekhe wa mikoa, Mashekhe wa wilaya, Mashekhe wa kata, Maimamu, Mashekhe wa taasisi zote nchini, na Waislamu wote kwa jumla, tufunge siku tatu kwanza, na tumuombe Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Ta’ala katika hizo siku tatu atuondoshee mabalaa na majanga makubwa, na madhara yanayotarajiwa kutokana na madhara makubwa ya mvua ya El Nino,” amesema.

Aidha, Mufti Mkuu amewaomba Waislamu kumuomba Mwenyezi Mungu afanye mvua hizo kuwa mvua ya rehema na yenye manufaa kwa jamii, badala ya kuwa chanzo cha adhabu na maafa.

“Na tumuombe Mwenyezi Mungu aifanye kuwa mvua ya rahma, mvua nzuri, isiwe mvua ya adhabu. Na atuondoshee aina zote za majanga na mabalaa,” amesema.

Amehitimisha kwa kusisitiza umuhimu wa kufunga na kuomba dua kwa pamoja ili kuiomba Tanzania kulindwa dhidi ya madhara yanayoweza kutokana na mvua hizo.

“Tufunge siku tatu, tumuombe Mwenyezi Mungu atuondoshee majanga yanayotarajiwa kutokana na madhara ya mvua ya El Nino.”

CHANZO:TRT Afrika