Mume wa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amefariki dunia leo kisiwani Zanzibar akiwa na umri wa zaidi ya 70
Taarifa za kifo cha Hafidh Ameir Hassan zimetangazwa rasmi na Makamu wa Rais wa nchi hiyo Deogratius Ndejembi, ambae amesema kuwa, kimetokea katika Hospitali ya Mzena iliyopo Zanzibar alipokuwa anapatiwa matibabu ya moyo.
Kwa mujibu wa Ndejembi, taratibu za mazishi zinaendelea.
Wakati huo huo, Rais wa Kenya William Ruto, kupitia ukurasa wake wa X, amesema kuwa amepokea taarifa za msiba kwa masikitiko makubwa.
"Rais Samia amempoteza mwenza wake wa maisha, watoto wake wamepoteza baba mpendwa, na Tanzania imepoteza mwananchi wao mahiri. Kenya iko pamoja na ndugu zetu wa Tanzania katika kipindi hiki cha majonzi," amesema Rais Ruto.
Nae Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye amesema Burundi inaungana na Tanzania katika kipindi hiki cha msiba.
"Kwa niaba yangu binafsi, na kwa niaba ya serikali na wanachi wa Burundi, natoa salamu zangu za rambirambi kwa Rais Samia, familia yake na wananchi wa Tanzania," amesema Rais Ndayishimiye.
Hafidh Ameir Hassan ambae ana watoto wanne na Rais Samia amefariki akiwa na umri wa zaidi ya miaka 70.
Akitoa salamu zake za pole Rais wa Zanzibar Hussein Ali Mwinyi alisema ‘‘amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za msiba huo na kuungana na Rais Dkt. Samia, familia, ndugu, jamaa, pamoja na wote walioguswa na msiba huo.’’
Rais Mwinyi pia alisema kuwa mazishi yatafanyika leo Jumatatu Septemba 7 eneo la Kizimkazi, Zanzibar.





















