Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, ameonya dhidi ya hatua za uhasama zinazolenga kuizunguka nchi hiyo, akisema Uturuki haitaruhusu safari yake ya kuwa taifa huru na lenye mafanikio kuzuiwa.
"Msimamo wetu wa utulivu na heshima usimfanye yeyote aelekeze mawazo yake kwingineko. Katika ardhi hii ambayo tumeifanya kuwa nchi yetu kwa kujitolea damu na maisha yetu, hatutamruhusu yeyote kuendesha operesheni yoyote," amesema Erdogan siku ya Jumatatu baada ya kikao cha Baraza la Mawaziri katika Ikulu ya Rais jijini Ankara.
“Hatutakaa pembeni na kutazama hatua za uhasama zinazolenga kuizunguka nchi yetu katika eneo letu. Uturuki hailengi nchi yoyote, jamii yoyote, imani yoyote wala utamaduni wowote,” amesema.
“Tunahitaji kuendelea na safari yetu kama taifa huru na lenye mafanikio katika eneo hili la kijiografia lenye mazingira magumu. Hatutaruhusu kamwe safari hii izuiwe,” Erdogan ameongeza.
“Wale wanaokerwa na kuimarika kwa nchi yetu na juhudi zetu za kuleta amani na utulivu katika eneo letu hawawezi kuturudisha nyuma katika njia yetu,” amesema.
Muungano na umoja
Erdogan pia amesema: “Tumeazimia kufanya kazi kuhakikisha kuwa umoja na mshikamano vinakita mizizi katika eneo letu pana, kwa kuzingatia sera yetu ya muungano na umoja.”
Akizungumzia kuhusu tukio la kuzama kwa meli lililotokea wiki iliyopita katika pwani ya mji wa Girne, katika Jamhuri ya Kituruki ya Kupro ya Kaskazini (TRNC), Erdogan alisema: “Kwa ushirikiano na TRNC, kwa sasa tunaunga mkono juhudi za utafutaji kwa kutumia meli tisa na ndege 11.”
"Tutaendeleza uhusiano wetu na Muungano wa Ushirikiano wa Shanghai, ambalo tunaliona kuwa linakamilisha juhudi za Umoja wa Mataifa," ameongeza Erdogan, akizungumza kufuatia mkutano wa kilele wa shirika hilo uliofanyika wiki iliyopita nchini Kyrgyzstan, ambapo alihudhuria kama mgeni wa heshima.
“Uongo na hujuma” za Israel zilikwamisha juhudi za amani
Akizungumzia migogoro ya kikanda, Erdogan aliilaumu Israel kwa vita vinavyoendelea Mashariki ya Kati pamoja na madhara yake mapana.
“Gharama ya vita vilivyoanza kutokana na njama na uchochezi wa Israel hailipwi na wananchi wa Iran pekee, wala nchi ndugu za Ghuba pekee, bali inalipwa na kila mtu, awe amehusika au la,” alisema.
Pia aliishutumu Israel kwa kudhoofisha makubaliano yaliyofikiwa mwezi Juni kwa ajili ya kumaliza vita.
“Kwa mara nyingine tena, ni uongo na hujuma za Israel ambazo zimefanya makubaliano ya Islamabad yashindwe kuwa na ufanisi, makubaliano ambayo yalileta nafuu kwa eneo letu lote,” Erdogan alisema.
Uturuki itaendelea na kuimarisha uchumi wake
"Dhoruba ya migogoro katika eneo letu haitatulia hadi pale mtazamo huu wenye msimamo mkali—unaoliona hata wazo dogo la amani kuwa tishio—utakapobadilika," Rais wa Uturuki aliongeza.
Licha ya mvutano wa kikanda, Erdogan alisema Uturuku itaendelea na mpango wake wa kiuchumi.
“Ingawa tunafanya baadhi ya marekebisho katika malengo yetu, tunaendelea kuuweka uchumi wa Uturuki katika njia ya maendeleo na ukuaji,” alisema.
“Tutaendelea kuchukua hatua zitakazoongeza ustawi wa taifa letu na kutoa suluhisho la kudumu kwa matatizo ya kimuundo ya uchumi wetu,” Erdogan alisema.
“Tutafanya kila kinachohitajika ili kuufanya uchumi wa Uturuki kuwa imara zaidi, wenye ushindani zaidi na wenye uwezo mkubwa wa kustahimili misukosuko katika kila eneo,” aliongeza.






















