Urusi na Ukraine wameshambuliana kwa droni usiku kucha hadi Ijumaa, huku mashambulizi yakilenga maeneo ya mbali katika mstari wa mbele na kusababisha vifo, uharibifu na moto kwa pande zote mbili.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy anasema droni ya Urusi imelenga makao makuu ya Usalama ya Ukraine, SBU, katika mtaa wa Volodymyrska katikati mwa mji wa Kiev, ikilenga hasa ofisi ya mkuu wa idara hiyo.
Meya wa Kiev Vitali Klitschko anasema watu watano walijeruhiwa, huku moshi mweusi ukionekana katika eneo la karibu la Kanisa la St. Sophia. Taarifa za hivi karibuni zimethibitisha kuwa mashambulio hayo yalikuwa sehemu ya mashambulizi makali ya Urusi kwa mji mkuu wa Ukraine.
Katika kanda ya kusini ya Odessa, mtu mmoja aliuawa na wengine watano kujeruhiwa katika mashambulizi ya usiku ya Urusi, Gavana wa kanda hiyo Oleh Kiper alisema.
Mashambiulizi hayo yaliharibu miundombinu ya raia, ikiwemo majengo ya umma na binafsi na magari ya serikali, alisema.
Jeshi la Anga la Ukraine linasema Urusi ilirusha droni 121 na kombora moja, na kudai kutibuwa zile zilizolenga maeneo 103 kote nchini.
Ukraine yashambulia miundombinu ya nishati ya Urusi
Wakati huohuo, Mamlaka za Urusi zimeripoti mashambulizi makubwa ya Ukraine katika mji wa kitalii wa Bahari Nyeusi wa Sochi na maeneo ya karibu ya Sirius.
Mashambulizi hayo pia yalisababisha moto katika kituo cha mafuta, kulingana na makao makuu ya operesheni ya kanda ya Krasnodar.
Awali hakukuwa na taarifa zozote kuhusu waliouawa, huku mamlaka zikisema kuwa majengo ya makazi ya watu na maeneo mengine yaliharibiwa.
Wizara ya ulinzi ya Urusi inasema mifumo yake ya ulinzi ya anga imeharibu droni 490 za Ukraine katika eneo la Urusi, na lile lilomegwa na Urusi la Crimea na Bahari Nyeusi katika mashambulizi hayo ya usiku.
Urusi pia inadai vikosi vyake vilishambulia kile inachosema kuwa ni eneo la kijeshi la Ukraine pamoja na maeneo ya nishati, ikiwemo kituo kimoja cha kupata mikakati eneo la Kiev, meli ambazo zinadaiwa kubeba silaha katika bandari ya Yuzhny, na kituo cha mafuta cha Chornomorsk.
Madai haya hayakuweza kuthibitishwa kutoka kwa vyanzo huru.





















