Wizara ya Ulinzi ya Uturuki imeshtumu mashambulizi ya kijeshi ya Israel katika kanda, ikidai kuwa wanakiuka uhuru wa mipaka ya Syria na Lebanon na kutatiza usalama wa kanda na dunia.
Akizungumza katika mkutano wa kila wiki wa waandishi wa habari katika Kituo cha Ozdemir Bayraktar, Rear Admiral Zeki Akturk alisema Israel inaendeleza kile alichokieleza kuwa “ulowezi wa kigaidi” Palestina na kufanya uchokozi unaokiuka historia na uhalali wa maeneo Matakatifu ya Waislamu Jerusalem Mashariki inayokaliwa.
Kulingana la Akturk, sera za Israel ni hatari siyo tu kwa amani na usalama wa kanda lakini pia kwa usalama duniani, huku ikitilia doa imani kwa sheria ya kimataifa miongoni mwa watu kote katika kanda.
Uturuki itaendelea na juhudi za kuimarisha amani na usalama, Akturk alisema, huku akitoa wito kwa jamii ya kimataifa kuchukua hatua madhubuti dhidi ya kile alichokieleza kuwa mtazamo wa Israel wa “upanuzi na mauaji ya halaiki”.
Uturuki yakanusha madai kuhusu wanachama wa kigeni kundi la SDF
Wizara hiyo pia ilikanusha taarifa kuwa wanachama wa kigeni wa kundi la kigaidi linaloongozwa na YPG la SDF wataondoka Syria na kwamba baadhi yao watasafiri hadi Uturuki.
Katika taarifa iliyotolewa, wizara hiyo ilisema kuwa inafuatilia kwa karibu yanayojiri kuhusiana na mchakato unaolenga kulinda uhuru wa mipaka ya Syria na msimamo wa “taifa moja, jeshi moja”.
“Madai kuwa wanachama wa kigeni wa SDF wataondoka Syria na kwamba baadhi yao watakuja Uturuki hayana ukweli wowote,” wizara ilisema.
Ilitoa wito kwa vyombo vya habari na umma kutozipa uzito taarifa hizo na maelezo yoyote kuhusu suala hilo ambazo hazitoki rasmi katika wizara.
Uturuki na Syria yakamilisha daraja la pili la baharini
Akturk anasema Uturuki na Syria wanaendelea na juhudi za kuchangia usalama na kurudisha ya hali ya kawaida nchini Syria.
Daraja la pili la baharini katika mto Euphrates, lilojengwa kwa pamoja na jeshi la Uturuki na Syria, lilikamilika tarehe 30 Agosti, alisema.
Daraja hilo linachukua nafasi ya kivuko kilichoharibiwa na mafuriko na linatarajiwa kurahisisha usafiri katika kingo hizo mbili za Euphrates.
Akturk alieleza kuwa mradi huo ni ishara ya ushirikiano na umoja kati ya majeshi ya Uturuki na Syria.
Mafunzo kwa marubani wa Eurofighter kuanza tarehe 7 Septemba
Akturk anasema mchakato wa manunuzi wa ndege za kijeshi za Eurofighter unaendelea na Uingereza ili kukamilisha masharti yanayohitajika ya Jeshi la Anga la Uturuki.
Wizara hiyo inasema marubani wa Uturuki wameanza mafunzo mwezi Agosti kama sehemu ya mpango huo wa manunuzi.
Marubani wamekamilisha mafunzo ya awali na wanatarajiwa kuanza kurusha ndege kuanzia tarehe 7 Septemba 2026. Mafunzo ya kuendesha ndege yatakuwa kwa miezi minane, yakifuatwa na miezi mitatu ya mkufunzi wa marubani.
Marubani wa Uturuki wataendelea kupelekwa Uingereza kwa mafunzo kwa awamu, kulingana na wizara hiyo.
Mamlaka za Somalia zaokoa meli iliyokuwa imetekwa nyara
Wizara hiyo pia ilieleza kuhusu meli iliyokuwa imetekwa nyara na maharamia katika bahari ya Somalia.
Inasema kuwa Uturuki ilitoa msaada muhimu kwa mamlaka za Somalia kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki kwa misingi ya makubaliano kati ya mataifa hayo mawili.
Kufuatia operesheni hiyo iliyofanywa na mamlaka za Somalia, maharamia hao waliondoka kwenye chombo hicho na meli ikapatikana salama, wizara hiyo ilisema.
Uturuki, Pakistan na Saudi Arabia yaimarisha ushirikiano wa ulinzi
Wizara hiyo ilieleza kuhusu muundo wa Muungano wa Ulinzi wa Makkah uliowahusisha Uturuki, Pakistan na Saudi Arabia.
Mawaziri wa Ulinzi na mambo ya nje, pamoja na wakuu wa majeshi kutoka nchi zote tatu, walikutana jijini Istanbul tarehe 31 Agosti kujadili hatua za ushirikiano wa kuweka utaratibu wa kitaasisi katika muungano huo.
Nchi hizo tatu zimekubaliana kuanzisha sekretariati nchini Saudi Arabia ikiongozwa na katibu mkuu. Maafisa kutoka mataifa hayo matatu watahudumu katika nafasi kwa kupokezana, huku Pakistan ikianza kwa katibu mkuu wa kwanza kwa kipindi cha miaka mitatu.
Muungano huo unatarajiwa kuangazia mipango ya pamoja ya kijeshi,mafunzo na mazoezi, pamoja na kuimarisha mawasiliano miongoni mwa majeshi ya nchi hizo tatu.
Ushirikiano katika sekta ya ulinzi utajumuisha uzalishaji wa pamoja, kuendeleza teknolojia na kubadilishana utaalamu.
Wizara inasema taratibu hizo zitaimarisha uwezo wa ulinzi wa muungano huo na kinga wakati ikichangia katika amani na usalama wa kanda.






















