Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amewatuhumu maafisa wa usalama kwa kushindwa makusudi kumwamsha asubuhi ya shambulio la ghafla la tarehe 7 Oktoba—siku moja baada ya mkewe kudai kuwa kiongozi mmoja wa upinzani alikuwa na taarifa za awali kuhusu shambulio hilo.
Netanyahu anakabiliwa na uchaguzi wenye ushindani mkali baadaye mwaka huu na anakabiliwa na ukosoaji endelevu kuhusu dhima yake katika mapungufu ya kiusalama yaliyohusishwa na tukio la tarehe 7 Oktoba 2023.
Ingawa hapo awali waziri mkuu alidai kuwa maafisa walijizuia kumwamsha, sasa anadai kuwa uamuzi huo ulifanywa kwa makusudi.
"Kwa nini hawakuniamsha? Kwa sababu walijua kwamba mimi, kama Waziri Mkuu wa Israel, ningeagiza mara moja jeshi zima liwe katika hali ya tahadhari na miji yote iwe macho... Jambo hili limefichwa kutoka kwa umma," alisema Netanyahu wakati wa matangazo kwenye mtandao wa Instagram.
Katika mahojiano tofauti, Netanyahu aliwalaumu viongozi wakuu wa jeshi na mkuu wa zamani wa shirika la usalama la Shin Bet, Ronen Bar, akidai kuwa walizuia taarifa za tahadhari ili kuepuka kuchochea mzozo wa kijeshi.
Madai ya njama
Matamshi hayo yalifuatia mahojiano ya televisheni na mkewe Sara kwenye Channel 14, ambapo alidai mpinzani Yair Golan alikuwa anajua mipango ya shambulio awali.
Golan, ambaye anaongoza chama cha Democrats cha mrengo wa kati kushoto na aliyekimbilia kusini mwa Israel mnamo Oktoba 7, alitishia kuwasilisha kesi na kudai sheki milioni 2.5 ($830,000) ya kashfa isipokuwa mke wa Netanyahu aombe msamaha mara moja.
"Sara Netanyahu alieneza njama ya uongo katika jaribio la kuandika upya Oktoba 7, na kuwafanya wale waliotoka kuokoa maisha kuwa wasaliti," Golan alisema.
Mkuu wa zamani wa jeshi Gadi Eisenkot, mpinzani mkuu wa uchaguzi, alilaani madai hayo kama "njama ya usaliti wa kichaa."
Kura ya maoni ya Agosti ilionyesha asilimia 40 ya Waisraeli na asilimia 63 ya wapiga kura wa muungano wa mrengo wa kulia wanaamini uhaini wa ndani ulichangia shambulio la kushtukiza ya Oktoba 7.


















