| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
Mgomo wa wafanyakazi katika uwanja wa ndege waathiri usafiri nchini Kenya
Muungano wa Wafanyakazi wa Usafiri wa Anga Kenya (KAWU) ulisema mgomo huo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta umetokana na malalamiko kadhaa, yakiwemo masuala ya ajira.
Mgomo wa wafanyakazi katika uwanja wa ndege waathiri usafiri nchini Kenya
KAA ilisema siku ya Jumapili kuwa baadhi ya safari za ndege zilikuwa zikikumbwa na ucheleweshaji, bila kutoa sababu za ucheleweshaji huo. / / Reuters

Safari za ndege katika uwanja mkuu wa kimataifa wa Kenya siku ya Jumatatu zimeathiriwa, huku maelfu ya wasafiri wakikumbwa na ucheleweshaji kutokana na mgomo wa wafanyakazi wa uwanja huo ulioingia siku yake ya pili. Muungano mkuu wa wafanyakazi umesema kuwa mazungumzo ya kutafuta suluhu yanaendelea.

Muungano wa Wafanyakazi wa Usafiri wa Anga Kenya (KAWU) ulisema mgomo huo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta umetokana na malalamiko kadhaa, yakiwemo kushindwa kukamilisha makubaliano ya pamoja ya majadiliano ya masuala ya ajira kati ya muungano huo na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Kenya.

Pia, muungano huo ulilalamikia ukosefu wa ushirikiano kutoka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Kenya (KAA) na Kenya Airways, pamoja na kampuni yake tanzu ya Jambojet.

KAA ilisema siku ya Jumapili kuwa baadhi ya safari za ndege zilikuwa zikikumbwa na ucheleweshaji, bila kutoa sababu za ucheleweshaji huo. Mamlaka hiyo haikutoa ufafanuzi wowote kwa Shirika la Habari la Reuters siku ya Jumatatu. Mamlaka ya Usafiri wa Anga Kenya pamoja na Jambojet pia hazikujibu maombi ya kutoa maoni.

Shirika la taifa la ndege la Rwanda, RwandAir, lilisema katika chapisho kwenye mtandao wa X siku ya Jumapili kuwa limefuta safari mbili za ndege kutokana na kile lilichokiita changamoto za udhibiti wa trafiki ya anga katika uwanja wa ndege wa Nairobi.

Abiria waliiambia Reuters kuwa walitumia saa kadhaa katika uwanja huo wakisubiri taarifa kuhusu safari zao za ndege.

“Nilipofika hapa, niliambiwa safari ya ndege imecheleweshwa hadi saa 7:00 usiku. Hiyo ilikuwa ni kuchelewa kwa saa moja na nusu, kisha kukawa na ucheleweshaji mwingine hadi saa 10:30 alfajiri. Takribani saa 9:00 usiku, nilikwenda kwenye eneo la usajili wa abiria, ndipo nikaambiwa kuwa safari hiyo imefutwa,” alisema Rabbi Mendel Goldman, ambaye alikuwa akisafiri kwenda Florida kuhudhuria harusi.

“Safari ya mapema zaidi wanayoweza kutupatia ni kesho usiku, hivyo tunalazimika kusubiri,” Goldman alisema Jumatatu. “Tutajaribu kutumia muda huu kwa namna bora iwezekanavyo, lakini kwa sasa nimekuwa hapa kwa saa 12 nikisubiri.”

Katibu Mkuu wa KAWU, Moss Ndiema, alisema muungano huo na maafisa wa serikali walikutana siku ya Jumapili ili kutafuta suluhu ya masuala yaliyosababisha mgomo, lakini hawakufanikiwa.

“Tumekubaliana kuendelea na mazungumzo kesho, kuanzia saa 5:00 asubuhi. Wakati huo huo, mgomo bado unaendelea,” alisema katika mahojiano yaliyorushwa na kituo cha televishe cha KTN siku ya Jumapili.

CHANZO:Reuters