Rais wa Burkina Faso, Ibrahim Traore, amehudhuria hafla ya kuhitimu kwa vijana 65,000 waliomaliza mafunzo ya lazima ya uzalendo nchini humo, huku akiwahimiza kufanya kazi kwa bidii ili kulinda uhuru na mshikamano wa taifa.
Serikali ya Traore ilianzisha mpango wa Mafunzo ya Lazima ya Uzalendo mwaka 2025, unaowataka wanafunzi wanaomaliza shule za sekondari kuhudhuria mafunzo ya mwezi mmoja yanayolenga kuwafunza maadili, uzalendo, nidhamu na uelewa wa historia. Baada ya mafunzo hayo, hupewa cheti ambacho ni sharti kwa ajili ya kujiunga na chuo kikuu.
Kiongozi huyo wa Burkina Faso aliwataka vijana hao kujenga na kudumisha unyenyekevu na uzalendo, huku wakijifunza kuielewa dunia pamoja na siasa za kimataifa.
“Mtu asiye na uelewa ni hatari kwa mabadiliko tunayoyapigania,” Traore amesema katika hafla hiyo siku ya Alhamisi, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ikulu.
“Haijalishi hali mnayokabiliana nayo, lazima mjitume… epukeni njia za mkato na kutafuta njia rahisi, kwa sababu njia hiyo inaelekea kwenye usaliti,” aliwaambia vijana hao wa Burkina Faso.
Hiki ni kikundi cha pili cha kuhitimu tangu kuanzishwa kwa mpango huo wa mafunzo ya lazima. Kwa mujibu wa mamlaka, mpango huo unalenga kuimarisha mshikamano wa kijamii na kujenga kizazi cha wananchi waliojitolea kuilinda na kuitumikia nchi yao.























